Mkurugenzi wa Tume ya Tehama Tanzania Samson Mwela amesema shughuli ya utoaji tuzo wa taasisi, makampuni na watu binafsi waliofanya vizuri kwenye matumizi ya TEHAMA itafanyika Oktoba 20 mkoani Arusha kwenye Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Tehama.
Amesema hayo wakati wa mahojiano katika kipindi cha Supa Breakfast cha East Africa Radio ambapo Mwele ameeleza kuwa tuzo hizo zinaanza mwaka huu na zitafanyika katika mkutano mkuu wa mwaka wa TEHAMA
”Hizi tuzo ndio tunazianzisha mwaka huu, na zinafanyika wakati wa mkutano mkuu wa mwaka wa Tehama ambapo kwa mwaka huu unafanyika Arusha kuanzia Oktoba 20 hadi 22 na tuzo zitatolewa hiyo Oktoba 20 kwa maana ya siku ya ufunguzi,” amesema Mwela.
”Tatakuwa na tuzo inaangalia masuala ya ubunifu na tafiti ambapo hapa kuna tuzo kama 6, mbunifu wa kike mwanafunzi, mbunifu wa kiume mwanafunzi, kuna mtafiti wa kike wa kiume wa Tehama na mtafiti wa kike wa Tehema”amesema Samson Mwela.
Aidha, ameeleza kuwa tuzo hizo zitagusa maeneo mbalimbali ikiwemo Vyombo vya Habari, Wanahabari, Wasanii, Taasisi za Kifedha, Taasisi za Serikali kwa maana ya Wizara, Wabunifu pamoja na Makampuni ya simu.
”Kuna eneo la huduma za habari tutaangalia chombo gani cha habari kinatumia vizuri zaidi tehama pia mwandishi gani wa habari anatumia vizuri sana tehama kwa mapana yake, hawa wote watapendekezwa na tutawatambua kama watu wanaosaidia ukuaji wa tehama,” amesema Mwela.
”Tuzo nyingine ni kwa hawa watoaji wa huduma za Tehama, makampuni ya simu, jamii yenyewe itaona imepata huduma nzuri kutoka kampuni gani itapendekeza ili sisi tutambue na kuweza kutoa tuzo. Pia kuna tuzo ya msanii anayetumia vizuri zaidi Tehama naye atapendekezwa”amesema Mwela.