Bondia wa Tanzania, Twaha Kiduku maarufu kama ‘Mzee wa Shosho’ amempiga mpinzani wake, Tshibangu ‘Beberiko’ Kayembe kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika pambano lililomalizika usiku huu jijini Dar es Salaam.
Wababe hao walikutana kwenye pambano lisilo na ubingwa la raundi nane lililovuta idadi kubwa ya mashabiki na kuoneshwa mubashara na kituo cha runinga cha Azam TV.
Majaji watatu wa pambano hilo wote walimpa ushindi Twaha Kiduku, wakimpa ushindi wa raundi 6 kati ya raundi 8 za pambano hilo.
Twaha alionekana akiwa tofauti katika pambano hilo, akiwa ametulia na kupiga kwa kutafuta alama za ushindi zaidi kuliko mtindo wake uliozoeleka wa kutumia nguvu zaidi.
Kayembe ambaye aliwahi kupigana na Hassan Mwakinyo na kupoteza pambano hilo, alikuwa bondia mgumu dhidi ya Twaha katika pambano hili, akionesha uwezo wa kuvumilia masumbwi mazito.
“Pambano lilikuwa zuri, namshukuru Mungu kwa sababu mpinzani wangu naye alijiandaa. Hii ni boxing huwezi kulazimisha kupata KO, nilijaribu lakini KO huja wakati wa mchezo ukiilazimisha utapata madhara,” alisema Twaha Kiduku.
Twaha alitumia nafasi hiyo kueleza kuwa tayari ameshasaini mkataba wa kukutana tena na Dullah Mbabe Juni 26, 2021. Katika pambano lao kwanza lililofanyika mwaka jana, Twaha alishinda kwa alama.
Kwa upande wa Kayembe, amesema kuwa ameridhika na uamuzi wa majaji wa pambano hilo na anajipanga kurejea tena ulingoni.