Bondia Twaha Kiduku ameahidi kubadilisha mfumo wa kuwachapa wapinzani wake kwa kutumia mfumo wa K.O baada ya kushinda mfululizo kwa mfumo wa pointi.
Bondia huyo wa Ngumi za Kulipwa nchini Tanzania ametoa ahadi hiyo akiwa katika maandalizi ya Pambano lake la Kimataifa dhidi ya mpinzani wake kutoka Georgia, Iago Kiziria.
Wawili hao wanatarajia kupanda ulingoni Aprili 22, kwenye Ukumbi wa Tanzanite uliopo mkoani Morogoro, likiwa pambano wa kwanza kwa Twaha Kiduku tangu kuanza kwa mwaka 2023.
Kiduku amesema kuwa moja ya malengo yake ni kuona anaweza kushinda kwa KO katika pambano hilo kwa kuwa mashabiki wake wamekuwa hawafurahii ushindi wake wa pointi anaoupata siku zote.
“Kwanza namshukuru Mungu, nimekuwa nikifanya maandalizi makubwa juu ya pambano langu na Kiziria kwa sababu najua halitokuwa pambano la rahisi hata kidogo kutokana na rekodi yake lakini nataka kuwaambia mashabiki wangu safari hii nitafanya balaa kubwa.”
“Unajua imekuwa ikiwakera wengi wakiona nikishinda kwa pointi na mabondia wote ambao nimekuwa nikiletewa wanakuwa siyo wepesi hata kidogo lakini safari hii niwahakikishie kwamba KO itahusika kuonyesha ubora wangu, mashabiki wangu naomba mjitokeze kwa wingi,” amesema Kiduku.