Timu ya taifa ya Wanawake ‘Twiga Stars’ ipo ugenini kucheza na Togo ikiwa ni mechi ya kuwania kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika (WAFCON) zitakazofanyika mwakani (2024) nchini Morocco na mastaa wa timu hiyo wameahidi kufanya vizuri.
Awali Twiga ilishinda mabao 3-0, mawili yakifungwa na Opah Clement na moja la kujifunga mchezo uliopigwa Novemba 30, Uwanja wa Azam Complex, Dar es salaam.
Staa wa JKT Queens na Twiga Stars, Stumai Abdallah amesema watapambana kuhakikisha wanashinda na kufuzu fainali ambayo hawajacheza muda mrefu.
“Tunaiona nafasi kubwa ya kushinda mchezo wa leo ilihali tupo ugenini, tayari tuna mtaji wa mabao kikubwa tutapambana kushinda na kusonga mbele” amesema Stumai Mchezaji wa BK Hacken ya Sweden.
Aisha Masaka amesema mchezo uliopita ulikuwa mgumu hasa kipindi cha kwanza kwani alikosa utulivu na kukosa nafasi nyingi lakini anaamini mchezo huo watafanya vizuri.
“Dakika 90 za mchezo uliopita zilikuwa ngumu, mimi mwenyewe sikuwa na utulivu kabisa licha ya timu kupata mabao mengi, tunaamini tuna nafasi ya kushinda na kwenda hatua nyingine ambayo ni Morocco.”
Mchezo huo ni muhimu kwa Twiga kwani ili kushiriki fainali hizo itatakiwa kufunga mabao au kuruhusu mabao mawili pekee, Twiga ni ukame wa miaka 13 kucheza michuano hiyo tangu iliposhiriki 2010.