Serikali imetoa Bonasi ya Sh. Milioni 200 kwa timu ya Taifa ya Wanawake ‘Twiga Stars’ baada ya kufuzu kushiriki Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON 2024).

Jumanne (Desemba 05), Twiga Stars ilifuzu Fainali za WAFCON kwa jumla ya mabao 3-2, ilishinda mabao 3-0 katika mechi ya Mkondo wa kwanza jjini Dar es salaam kabla ya kufungwa na Togo mabao 2-0.

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk. Damas Ndumbaro amesema Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ametangaza Bonasi ya Sh. Milioni 200 kwa wachezaji wa timu hiyo.

“Ushindi huu unaongea mambo mengi sana, kwanza soka la Tanzania limekua na uchumi unakua, sisi kama Serikali tutahakikisha tunawahamasisha watu wengi kusapoti michezo, kukuza na kutangaza utalii wa nchi yetu,” amesema.

Dk. Ndumbaro amesema katika nchi zote za ukanda wa CECAFA, Tanzania ndiyo nchi pekee iliyofuzu kwa wanawake na wanaume.

“Vijana hawa wanastahili pongezi sana, sisi kama Serikali tutajipanga kuhakikisha wanafanya vyema katika fainali za WAFCON zitakazofanyika mwakani nchini Morocco,” amesema.

Makamu wa Kwanza wa Rais Shirikisho la Soka Tanzania ‘TFF’, Athuman Nyamlani ameishukuru Serikali kwa kugharamia safari yote ya Twiga Stars.

Amesema hivi sasa Tanzania imepiga hatua katika soka pamoja na kuwa na wachezaji mahili.

“Tunaishukuru Serikali imetusaidia tiketi hadi kufika hapa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia Bonsai ya Sh. Milioni 200, pia dua za Watanzania zimesaidia,” amesema.

Nyamlani amesema soka ni mchezo wa maandalizi na kila siku huwa wanafanya maandalizi.

Ameongeza kuwa, hivi sasa soka la hapa nchini, limekomaa mpaka kuweza kuzitoa timu nzuri upande wa Afrika Magharibi.

Young Africans kujua mbivu na mbichi leo
Mahusiano: Huna jema la kuzungumza kaa kimya