Serikali ya Nigeria ilisimamisha Twitter Juni mwaka jana baada ya kampuni hiyo kufuta ujumbe wa Twitter wa Rais Muhammadu Buhari kuhusu kuwaadhibu wanaotaka kujitenga nchini humo.
Mamlaka zilishutumu kampuni hiyo ya mitandao ya kijamii kwa kuegemea upande wa watu wanaotaka kujitenga.
Lakini serikali ilisema inabadilisha marufuku hiyo baada ya Twitter kukubaliana na masharti ikiwa ni pamoja na kufungua ofisi ya ndani nchini Nigeria.
Hatua hiyo inaruhusu mamilioni ya watu katika taifa hilo lenye watu wengi zaidi barani Afrika kutumia mtandao huo tena.
Baadhi ya watumiaji walikuwa wameendelea kufikia tovuti hiyo baada ya kusimamishwa kwa kutumia mitandao ya kibinafsi (VPNs), lakini serikali iliapa kuwabana wale ambao bado wanatuma ujumbe kwenye Twitter, ikiwa ni pamoja na mashirika ya vyombo vya habari.
Hatua ya mwaka jana ya serikali ya Nigeria ilizua malalamiko ya kimataifa kuhusu uhuru wa kujieleza.
Uamuzi wa kampuni hiyo ya mitandao ya kijamii kujiandikisha nchini humo ulionyesha kujitolea kwa Nigeria, shirika la maendeleo ya teknolojia ya habari nchini humo lilisema.
Twitter bado haijatoa maoni yoyote kuhusu uamuzi wa Nigeria wa kuondoa marufuku hiyo.