Chama cha soka nchini England (FA), kimeliweka kapuni tukio la beki wa Man Utd, Marcos Rojo la kumkanyaga kiungo mshambuliaji wa Chelsea, Eden Hazard, tukio ambalo linadaiwa alilifanya kwa makusudi wakati wa mchezo wa robo fainali ya kombe la FA usiku wa kuamkia jana.
Vyombo vya habari vya England vililivalia njuga tukio hilo kwa kueleza kuwa Rojo alifanya kusudi kumkanyaga Hazard, hivyo alipaswa kufunguliwa mashtaka kama ilivyokuwa kwa beki wa AFC Bournemouth, Tyrone Mings.
Mings alifunguliwa mashtaka na kisha kufungiwa michezo mitano, baada ya kubainika alimkanyaga kwa makusudi mshambuliaji wa Man Utd, Zlatan Ibrahimovich wakati wa mchezo wa ligi ya nchini England.
Hata hivyo, Tyrone Mings ameonyesha masikitiko yake baada ya kuona FA wameshindwa kumfungulia mashtaka Marcus Rojo kwa kuandika katika mtandao wa kijamii wa Twitter.
Beki huyo ambaye tayari ameshatumikia adhabu kwa kukosa mchezo mmoja dhidi ya West Ham United uliochezwa mwishoni mwa juma lililopita, ameandika katika mtandao huo kwa kuonyesha hisia za kuchukizwa na maamuzi hayo.
Ameandika… “Lol.” “Nimesikitishwa sana na maamuzi yaliyochukuliwa dhidi yangu, lakini naona imekua tofauti kwa wengine ambao wamefanya kosa ambalo limeniweka pembeni kwa muda.”