Kiu ya kusikia kengele ya kuamuru kuanza kwa pambano kati ya mabingwa wa masumbwi wa dunia uzito wa juu, Tyson Fury na Deontay Wilder imekolezwa baada ya wababe hao kukutana uso kwa uso ulingoni na kutangaza kuzichapa huku kila mmoja akitamba.
Wilder alikuwa mmoja kati ya watazamaji wa pambano kati ya Tyson Fury na Francesco Pianeta usiku wa kuamkia leo, ambapo alishuhudia Fury akishinda huku akitawala pambano hilo.
Wakizungumza uso kwa uso baada ya Fury kutangazwa mshindi, Wilder alianza kwa kutamba akieleza wazi kuwa watapigana mwaka huu na kwamba atamzimisha mbabe huyo kutoka Uingereza.
Fury alijibu mashambulizi ya maneno akiwaahidi mashabiki 25,000 waliohudhuria pambano hilo kuwa ataenda Marekani kuzichapa na Wilder na kwamba atashinda kwa KO na kurejesha nyumbani mkanda wa WBC.
Hata hivyo, baada ya tambo hizo, Fury alizungumza tena na waandishi wa habari na kueleza kuwa pambano kati yake na Wilder litakuwa pambano gumu zaidi kwenye historia ya maisha yake.
Promota wa pambano hilo, Frank Warren amesema kuwa taarifa zaidi kuhusu wapi na lini pambano hilo litafanyika zitatolewa wiki ijayo, lakini itakuwa mwaka huu.
Wilder, mbabe ambaye hajawahi kupoteza pambano lake, amedai kuwa kwa mara ya kwanza Fury atapata uzoefu wa maumivu ya kupigwa KO. Fury anakuwa bondia anayepewa nafasi ndogo kulinganisha na Wilder kwenye pambano hilo, lakini historia ya kumshinda Wladimir Klitschko.