Mzizi wa fitna kati ya Tyson Fury na Deontay Wilder umekuwa mgumu kukatwa asubuhi hii, baada ya wababe hao kutoa sare katika pambano lao litakaloandikwa kwenye historia ya masumbwi kwa jinsi mambo yalivyobadilika ghafla.

Fury ambaye alikuwa anaonekana kuwa mbele kwa alama nyingi zaidi, akimpita Wilder hadi katika raundi ya 8, alijikuta akipigwa chini mara mbili katika raundi ya 9, lakini alifanikiwa kuamka.

Hata hivyo, akiwa anakaribia kusherehekea ushindi wake, aliingia tena kwenye mtego wa ngumi nzito ya Wilder dakika mbili kabla ya kumalizika kwa pambano hilo na kupigwa chini vibaya kiasi cha wengi kuamini hataweza kuamka.

Fury aliamka kwa kujikokota na kufanikiwa kumaliza raundi zote 12, akiokolewa na alama alizokuwa amezikusanya kabla ya raundi ya tisa ya pambano hilo.

Majaji wa pambano hilo lililohudhuriwa na watu zaidi ya milioni 18, wawili walitofautiana wakipeleka ushindi kwa Wilder na Fury lakini mmoja alitoa sare na kufanya uamuzi kuwa sare (115-111 Wilder, 114-110 Fury, 113-113 Sare).

Pambano hili limewashangaza wengi kwa jinsi ambavyo matokeo yake yamebadilishwa na raundi chache tofauti na wengi walivyokuwa wanatarajia.

Mcheza kikapu maarufu wa NBA, LeBron James ni mmoja kati ya waliopigwa na butwaa kwa walichokiona. Kupitia tweet yake, ameandika kuwa hilo lilikuwa pambano la raha na la aina yak ambalo hajawahi kuliona katika maisha yake, asiamini kilichotokea.

Kwa mantiki hiyo, Wilder amefanikiwa kutetea ubingwa wake na harufu ya pambano la marudiano imeanza kupata nafasi zaidi.

Mbabe wa masumbwi ya uzito wa Welterweight, Manny Pacquiao naye amekuwa mmoja kati ya walioeleza kuvutiwa na pambano hilo na kutamani kuona pambano la marudiano.

 

Bodi ya Filamu yampa Wema ‘hadidu za rejea’ kumtoa kifungoni
Video: Mwakyembe awapa 'neno' wasanii, makampuni uzinduzi Starline Films