Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko amewataka Wachimbaji wa Madini ya Viwandani na Ujenzi kuwa waaminifu katika kazi zao ili kukuza uchumi wa Taifa, ikiwemo kuzingatia ubora wa madini yanayopelekwa viwandani.
Dkt. Biteko ameyabainisha hayo jijini Dar es Salaam katika mkutano wa Wachimbaji Wadogo wa Madini na Wadau wa Madini ya Viwandani, huku akisema “hakuna mtu ambaye ana akili yake mwenye kiwanda ataamua kuagiza malighafi kutoka nje ya nchi kama malighafi hiyo anaipata hapa nyumbani kwa bei nafuu na kwa unaostahili.”
Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko
Aidha, katika hatua nyingine, Shirika la Madini la Taifa – STAMICO, limesaini hati za makubaliano na Kampuni ya Appollo, JF Trucks pamoja na Benki ya Azania, kushirikiana kwenye teknolojia, vifaa vya uchimbaji madini na fedha, mtawalia, vitakavyotumika kukuza uchimbaji wa madini ya viwandani na uchakatwaji wa bidhaa zake.
Zoezi hilo pia lilishuhudiwa na Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko ambapo utiaji saini wa makubaliano hayo uliofanyika jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano wa Wachimbaji wadogo wa Madini na Wadau wa Madini ya Viwandani.