Serikali imeanzisha vituo 26 vya ununuzi wa madini na kutoa jumla ya leseni tano za uchenjuaji wa madini ambapo jumla ya shilingi bilioni 409.66 sawa na asilimia 85.43 ya lengo la shilingi bilioni 479.51 zilikusanywa kutokana na mrabaha, ada ya ukaguzi, mauzo ya madini kwenye masoko na vituo na ada ya leseni za uchimbaji.
Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa jijini Dodoma nakuongeza kuwa katika mwaka 2023/2024, Serikali itaendelea kuhamasisha biashara na uwekezaji katika sekta ya madini na kuwaendeleza wachimbaji wadogo.
Amesema, ” Serikali pia itaendelea kuhamasisha shughuli za uongezaji thamani madini; kusimamia mifumo ya ukaguzi wa shughuli za migodi; na kuzijengea uwezo taasisi zinazosimamia sekta hiyo.”
Aidha, Majaliwa ameongeza kuwa, Serikali imeendelea kutekeleza azma yake ya kuimarisha shughuli za kiuchumi na kijamii kwa kuhakikisha wananchi wake wanapata nishati ya umeme, mafuta na gesi kwa uhakika na bei nafuu.