Sakata la Faru John linaendelea kuchukua sura mpya kila kukicha, baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kueleza kutoridhishwa na ripoti ya Wizara ya Maliasili na Utalii kuhusu kuhamishwa, kuugua na kufa kwa faru huyo.

Waziri Mkuu aliibua sakata hilo alipokuwa ziarani mkoani Arusha, ambapo alitaka apewe ripoti kamili ya sababu za kuhamishwa kwa Faru John kutoka hifadhi ya Bonde la Ngorongoro kwenda Grumeti, kuugua na kufa kwake.

Kwa mujibu wa taarifa ya ripoti iliyochapishwa na Mtanzania iliyowahoji maafisa kadhaa wa hifadhi hiyo, imeelezwa kuwa tabia korofi za faru huyo ndizo zilizopelekea Wizara kuridhia kuhamishwa kwake ili kunusuru wenzake.

Imeelezwa kuwa tabia hizo za Faru John zilipelekea kamati mbalimbali za watendaji wa hifadhi wakiwemo Mkuu wa Mamlaka ya Bonde la Ngorongoro, Dk. Fadhili Manongi, Mkurugenzi wa Utafiti wa Wanyama Pori, Dk. Simon Mduma na wengine kuridhia kuhamishwa kwake kutokana na sababu za kitaaluma.

Kabla ya kuchukua uamuzi wa kumhamisha, imeelezwa kuwa vigogo hao wa hifadhi hiyo waliwasilisha nyaraka zote za maamuzi hayo katika Wizara ya Maliasili na Utalii ambayo pia ilijiridhisha na kuridhia uhamisho huo.

Baadhi ya wahifadhi waliohojiwa, wameeleza kuwa Faru John ambaye alizaliwa katika hifadhi ya Ngorongoro alianza kuonesha tabia korofi hasa kwa faru wenzake dume.

Aidha, alieleza kuwa faru huyo alimuua faru mmoja jike kwa kumchoma na pembe, na pia kumuua faru mwingine dume katika mapigano.

“Tatizo lingine lililotokana na ubabe wa Faru John, ni gharama kubwa za ulinzi wa faru waliokimbia mapigano dhidi yake na kutawanyikahadi kwenye mashamba ya watu,” alisema mhifadhi mmoja ambaye hakutajwa jina.

Mhifadhi mwingine alieleza kuwa Faru John ambaye alikuwa na watoto wengi zaidi ndani ya hifadhi hiyo alianzisha tabia ya kuwapanda watoto wake, tabia ambayo kitaalam ingehatarisha maisha ya faru wengine.

“Faru John alianza kuwapanda watoto wake, jambo ambalo kitaalam sio salama kwa uhai wa faru, hivyo kuendelea kumwacha pale kreta lilikuwa jambo la hatari,” Mhifadhi mwingine anakaririwa.

Hata hivyo, licha ya kukiri kuwa ofisi yake ilipokea barua kutoka kwa uongozi wa Hifadhi ya Bonde la Ngorongoro kuhusu uamuzi wa kumhamisha Faru John, Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe aliwataka waandishi kusubiri majibu ya Kamati Maalum iliyoundwa na Waziri Mkuu.

“Ni kweli hiyo nyaraka ipo, lakini hili suala la faru John linafanyiwa kazi na vyombo vya dola. Nadhani sio vizuri kulijadili kwa undani sasa, tusubiri matokeo ya uchunguzi,” Profesa Maghembe anakaririwa.

Diamond atikisa Australia, wimbo wake wavunja rekodi ya mwaka
Waziri Nchemba atembelea WCB, aahidi kuongeza kasi ya kulinda kazi za wasanii