Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi – CCM Taifa, imeielekeza Serikali kuwachukulia hatua wahusika wote waliobainika kuhusika na ubadhirifu wa mali na rasilimali za nchi, ambao wametajwa kwenye ripoti ya  Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali – CAG na Taarifa ya Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa – TAKUKURU, kwa mwaka wa fedha 2021/22.

Hayo yamesemwa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM – Taifa, Itikadi na Uenezi, Sophia Mjema mara baada ya kikao  cha kawaida cha kamati kuu kilichoketi chini ya Mwenyekiti wa CCM Taifa, ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Amesema, Kamati Kuu imetoa maelekezo kwa Serikali kufuatilia Viongozi wanaoshindwa kuweka mbele uzalendo na maslahi ya nchi na kuongeza kuwa pia  kamati imepokea na kujadili kwa kina masuala mbalimbali ya kitaifa, ikiwemo Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali – CAG  na Taarifa ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa – TAKUKURU, zilizowasilishwa kwa Rais.

Aidha, Mjema amefafanua kuwa ilibainika kuwepo kwa maeneo ambayo taarifa zote mbili zimeonesha Serikali imeboresha na kuendelea kuimarisha kasi ya utoaji wa huduma kwa wananchi, ikiwemo udhibiti na umakini katika matumizi ya fedha za umma, kufuatia taasisi zilizokaguliwa, asilimia 96 kati yake zimepata hati safi.

Amesema, “katika mjadala huo wa kina Kamati imesikitishwa na kuwepo baadhi ya maeneo mengine ambayo bado yanatakiwa kufanyiwa kazi ili kuondoa mapungufu/udhaifu uliobainishwa, ikiwa ni pamoja na mifumo ya malipo na ukusanyaji wa mapato kutokusomana, kuwepo kwa baadhi ya watumishi wa umma wasiokuwa waadilifu.”

Simbachawene, Jenista wala kiapo Ikulu
Habari Kuu kwenye magazeti ya leo April 2, 2023