Viwango vya chini, vya ustadi wa somo la Hisabati hususani kwa wasichana, vimekuwa vikidhohofishwa na ubaguzi wa aina mbalimbali katika masomo na kusababisha watoto hao kushindwa au kukata tamaa ya kujiendeleza kimasomo.
Hayo, yamebainishwa katika ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto ulimwenguni UNICEF, ikiwa ni siku chache kabla ya kuanza kwa mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Marekebisho ya Mfumo wa Elimu kwa mataifa mbalimbali.
Ripoti hiyo, imesema wengi wa watoto hao, wameshuhudiwa kuwa na nia ya kujifunza masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati lakini wamekuwa wakikabiliwa na vikwazo mbalimbali ikiwemo kubaguliwa.
Imewataja miongoni mwa watoto hao, kuwa ni pamoja na Chantal Atovura ambaye ni mkimbizi kutoka nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), anayeishi nchini Sudan Kusini ambaye amesema, “ninapenda kemia na kama kuna nafasi ya mimi kuendelea na elimu, ningependa kusomea udaktari.”
Hata hivyo, ndoto za wasichana aina ya Chantal zinaweza kutoweka iwapo hatua hazitachukuliwa haraka na kila serikali kukomesha ubaguzi wa kijinsia, huku ripoti mpya iliyotolewa leo na UNICEF ikiwaweka nafasi ya nyuma wasichana katika somo la hisabati ikilinganishwa na wavulana.
Ripoti hiyo, iliyotolewa leo jijini New York nchini Marekani imepewa jina la “Tatua mlinganyo kuwasaidia wasichana na wavulana kujifunza hisabati,” ikitokana na utafiti kwenye zaidi ya nchi 100 duniani zenye uchumi wa chini na wa kati.