Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeikabidhi Takukuru jalada la kulifanyia uchunguzi upotevu wa fedha katika Ubalozi wa Tanzania nchini Ethiopia.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Faraji Mnyepe amekabidhi jalada hilo kwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Brigedia Jenerali John Mbungo katika ofisi ndogo za Wizara jijiji Dar es Salaam.
Hatua hiyo imekuja kutokana na jitihada za Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli za kupambana na kuzuia rushwa pamoja na matumizi mabaya ya fedha za umma.
Uchunguzi huo unafanyika baada ya kubainika upotevu/matumizi mabaya ya fedha katika Ubalozi wa Tanzania nchini Ethiopia.
Kuhusu kiwango cha fedha kilichopotea Katibu Mkuu, Dkt. Mnyepe, amesema kitajulikana mara baada ya Takukuru kukamilisha uchunguzi huo wa jalada walililokabidhiwa.