Hatimaye Timu ya Taifa ya Ubelgiji haitavaa jezi zao nyeupe za ugenini zenye neno “LOVE” kwenye kola katika mchezo wa hatua ya makundi ya Kombe la Dunia nchini Qatar, kufuatia majadiliano na Shirikisho la Soka Duniani ‘FIFA’.
Mazungumzo kati ya Shirikisho la Soka nchini Ubelgiji ‘RBFA’ yaliyochukua zaidi ya saa 24, yamefikia muafaka wa jezi hiyo kutotumiwa kwenye mchezo wa kesho dhidi ya Canada, na haitatumika kwenye Fainali zote za Kombe la Dunia mwaka huu 2022.
Ubelgiji ilizindua jezi zao za ugenini mwezi Septemba kama sehemu ya makubaliano na Kampuni ya Vifaa vya Michezo ya ADIDAS na tamasha la muziki Tomorrowland.
Kwa Maamuzi hayo, Timu ya Ubelgiji itavaa jezi nyekundu za nyumbani katika michezo yote ya hatua ya Makundi dhidi ya Canada, Morocco na Croatia.
Katika taarifa iliyotolewa na Kampuni ya vifaa vya Michezo ya ADIDAS imeeleza: “Kwa maamuzi ya kutotumika kwa Jezi za ugenini za Ubelgiji, kwa ushirikiao na Shirikisho la Soka nchini humo tunakusudia kutoa kauli chanya kuhusu neno ‘LOVE’ ambalo lilikusudia kusisitiza upendo mahala penye machafuko, na sio kuunga harakati za mapenzi ya jinsia moja.”
Ubelgiji ilivalia jezi za ugenini kwa mara ya kwanza katika mchezo wa Uefa Nations League ilipochapwa na Uholanzi mwezi Septemba.
Habari hizi zinakuja baada ya Uingereza, Wales na mataifa mengine ya Ulaya kuthibitisha kuwa hawatavaa kitambaa cha OneLove kwenye Kombe la Dunia kwa sababu ya tishio la wachezaji kupata kadi za njano.
Manahodha, akiwemo Muingereza Harry Kane na Gareth Bale wa Wales, walikuwa wamepanga kuvaa kitambaa hicho wakati wa michezo yao ya kwanza katika Fainali za Kombe la Dunia.