Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewaagiza wazalishaji wa Madini ya Chumvi nchini kuzalisha kwa wingi na kwa ubora ili kukidhi viwango vinavyohitajika katika soko la ndani na nje.
Amesema hayo, wakati akifunga Maonesho ya Kwanza ya Madini na Fursa za Uwekezaji mkoani Lindi Wilayani Ruangwa ambayo yalihusisha zaidi ya washiriki 140 kutoka ndani na nje ya nchi.
Waziri Mkuu Majaliwa amesema, lengo la maonesho hayo ni kutangaza fursa za Uwekezaji katika Sekta ya Madini zilizopo mkoani humo.
Aidha, ameitaka Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) kuendelea kufanya tafiti mbalimbali za madini ili kugundua maeneo mapya ya uchimbaji Madini kwa lengo la kuongeza wigo na fursa za ajira kwa Watanzania.
Sambamba na hayo, Majaliwa amesisitiza uongezaji thamani madini kufanyika nchini kwa lengo la kuzalisha bidhaa zenye ubora zinatokana na Madini na kuongeza ajira kwa Watanzania hivyo kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Kwa upande wake, Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ameipongeza Serikali kwa kuweka mazingira mazuri ya Uwekezaji na kuwataka wananchi wa Mkoa wa Lindi hususan Wilaya ya Ruangwa kutunza rasilimali zilizopo Mkoani humo ikiwemo ardhi.
Naye, Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko amesema Wizara ya Madini itaendelea kusikiliza maelekezo yanayotolewa na viongozi ili kuipeleka sekta madini mbele inayoongoza kwa kuliingizia Taifa fedha za kigeni kutokana na kuuza bidhaa za Madini.