Waziri wa Maendeleo ya Jami, Jinsia, Wanawake na Makundi maalum, Dkt. Dorothy Gwajima amesema Serikali imesema ubunifu wa miradi utasaidia vyuo vya Maendeleo ya Jamii kukusanya mapato zaidi na kujiendesha kwa kiasi kikubwa.
Dkt. Gwajima ameyasema hayo hii leo Agosti 23, 2023 jijini Dodoma wakati alipokuwa akijibu hoja mbele ya Kamati ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii wakati wa kikao na Kamati hiyo juu ya uendeshwaji wa chuo cha Maendeleo ya Jamii Rugemba.
Waziri Dkt. Gwajima amesema endapo Vyuo vya Maendeleo ya Jamii vitaweza kuwekeza katika ubunifu wa miradi mbalimbali itakuwa ni njia ya haraka ya wao kupata pesa ambazo zitawawezesha kujiendesha na kupunguza utegemezi Serikali kuu.
“Tukiwekeza kwenye miradi yetu kama kilimo, ufugaji na miradi mingine mingi kulingana na eneo husika kwa ubunifu na ustadi naamini tutaweza kuongeza kipato na kupunguza utegemezi wa fedha kutoka serikalini,“ alisema Dkt. Gwajima.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. John Jingu amesema suala la uanagenzi ni jambo linalofanyika katika Vyuo vyote vya Maendeleo ya jamii nchini ili kutoa wataalam wenye ujuzi watakaweza kuleta matokeo chanya kwa maendeleo ya Jamii na Taifa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii Mhe. Fatma Toufiq, ameishauri Serikali kushirikiana na wadau tofauti wa maendeleo kwenye kukuza miradi iliyopo katika Vyuo vya Maendeleo ya Jamii ili iweze kusaidia katika uendeshaji wa Vyuo hivyo.