Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amempa onyo Kaimu Meneja Mwandamizi wa Usafirishaji wa Umeme, wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Amos Kahiyula huku akiagiza kusimamishwa kazi kwa muongoza mifumo ya umeme wa kituo cha kupoza nishati hiyo kilichoko Ubungo jijijini Dar es Salaam, Samson Mwangalume.
Waziri Kalemani amefikia uamuzi huo baada ya kutoridhishwa na maelezo ya Kahiyula kuhusu sababu za kukatika mara kwa mara kwa umeme jijini Dar es Salaam jana usiku.
Kahiyula alimueleza Waziri Kalemani kuwa tatizo hilo la kukatika umeme limetokana na uchafu wa vikombe vinavyowekwa kwenye njia ya kusafirisha umeme huo.
Dkt. Kalemani alisema haridhishwi na sababu zilizotolewa na kueleza kuwa huo ni uzembe wa kutosafisha vikombe uliofanywa na afisa huyo wa Tanesco.
“Haiwezekani watu mkae muda mrefu bila kutazama hali ya vikombe hadi viwe vichafu kiasi cha kusababisha umeme kukatika, huu ni uzembe usiokubalika kwani Serikali imeshawekeza vya kutosha kuhakikisha umeme unakuwa wa uhakika,”alisema Dkt. Kalemani.
“Nataka huyo Samson aliyekuwa mkuu wa zamu ya asimamishwe kazi kuanzia leo na maelekezo yake ofisini kwangu kwani kama vikombe vipo kwanini hamkuviweka,” aliongeza Dkt. Kalemani.
Aprili mwaka huu, Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ilibainisha kuwa pamoja na mambo mengine alieleza kuwa usimamizi mbovu wa ununuzi wa vipuri kwa ajili ya matengenezo ya mitambo na kutofuatwa kwa mfumo wa ununuzi wa umma katika baadhi ya vituo ni chanzo cha kuwa na vipuri visivyoakisi thamani halisi ya fedha, na hivyo kupunguza ufanisi wa utoaji huduma ya umeme kwa wananchi.