Ikiwa imebaki takribani miezi tisa Watanzania washiriki Uchaguzi Mkuu, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Bashiru Ally amesema kuwa dhana ya wapinzani na mbinu wanazotaka kutumia ili kushinda uchaguzi huo ni kujidanganya.
Akizungumza na viongozi wa chama hicho, Ijumaa, Januari 17, 2020 katika Kata ya Kazuramiba wilayani Kigoma, Dkt. Bashiru amesema kuwa chama hicho kitawaomba kura wananchi kwa kutumia kazi iliyofanywa na Serikali inayoundwa na chama hicho.
Katibu Mkuu huyo wa CCM alisema kuwa wapinzani wanajidanganya kwa kudhani kuwa watatumia maneno ya uongo na bendera wakisubiri kura zishuke kama mvua.
“Kama wao wanadhani kura zitashuka kama mvua, au wanafikiri wakipita na kusema uongo wakijinadi na bendera wakati wa kampeni watapata kura wanajidanganya,” alisema Dkt. Bashiru.
Alieleza kuwa chama hicho kilianza kuomba kura kwa wananchi tangu mwaka 2015 kilipopewa dhamana ya kuunda Serikali, na kwamba kwa kutumia miradi iliyotekelezwa ya afya, miundombinu ya kisasa, shule, miradi ya maji, mradi wa umeme wa Stigler’s Gorge na mingine ni chanzo cha ushindi wa chama hicho mwaka huu.
Mwaka huu, Tanzania itafanya uchaguzi mkuu ambapo Rais John Magufuli anatarajiwa kugombea muhula wa pili, huku hali ikionesha kuwa hatakuwa na upinzani mkubwa kulinganisha na ilivyokuwa 2015.