Mwaka huu umeanza kwa hekaheka nzito kuwahi kushuhudiwa kwenye harakati za kisiasa kwenye uchaguzi mdogo wa wabunge ambao wameweka historia ya ‘wachezaji’ kubadili jezi za timu zao za awali na kucheza mechi ileile wakiwa upande wa waliokuwa wapinzani wao.
Hii ndiyo picha ya haraka unayoweza kuzipa chaguzi ndogo za majimbo ya Kinondoni na Siha, ambazo waliokuwa wabunge wake kwa tiketi ya vyama vya upinzani, Dkt. Godwin Mollel (Siha) na Maulid Mtulia (Kinondoni), walivyoamua kubadili gia angani, wakajiuzulu nafasi zao za ubunge na kuhamia CCM ambapo wamepewa nafasi ya kugombea katika majimbo yaleyale.
Katika hali hii, Chadema ambao ndio chama kikuu cha upinzani kilichoweka wagombea wake makini, Salum Mwalimu (Kinondoni) na Elvis Mos (Siha) ndio mabingwa watetezi wa majimbo hayo dhidi ya wapinzani wao wakuu Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanaowatumia watu walewale ambao Chadema waliwamwagia sifa nyingi na kufanikiwa mwaka 2015 katika majimbo hayohayo.
Nitawazungumzia Chadema zaidi kwani kama nilivyosema ndio mabingwa watetezi kwenye uchaguzi huu mdogo.
Nimeona tangu kipyenga kilipopulizwa kwa ajili ya uchaguzi mwingine wa marudio, Chadema wamekuwa wakilalamika sana kuhusu kilichotokea huku wakiwaita wagombea wa CCM kuwa ni wasaliti na hawafai kuaminika tena. Wameeleza kuwa watu hao wamewasaliti wananchi waliowaamini mwaka 2015.
Pia, hoja zilizotolewa na wabunge hao kuwa wamehamia CCM ili kumuunga mkono Rais Dkt. John Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya, imepata pingamizi kubwa, baadhi wakieleza kuwa wangeweza kumuunga mkono Mheshimiwa Rais wakiwa katika vyama vyao kwa wakati huu.
Hoja nyingine nzito ya Chadema ambayo imeshika kasi mitandaoni ni kwamba uchaguzi huo wa marudio ni ‘changa la macho’ kwani watu walewale wanarudi wakiwa wamebadili vyama na kwamba wameisababishia gharama ‘isiyo ya lazima’ ya takribani shilingi bilioni moja.
Na kwa uzito wa hoja hizo, kwamba kiasi hicho cha fedha ni kingi na kingeweza kutumika kujenga shule, zahanati au hata kuboresha miundombinu ya maji kwa wakaazi husika kwa kiasi kikubwa sana endapo wabunge haohao wangepewa kwa ajili ya jimbo husika.
Hizo ndizo hoja kuu za Chadema za awali ambazo zimepata umaarufu mitandaoni na huenda zikatumika pia kwenye kampeni kwa kiasi kikubwa.
Lakini, Chadema wanapaswa kuanza kufikiria nje ya sanduku (box) ya hoja hizo kwani ni rahisi kuweza kupanguliwa na wapinzani wao (CCM) ambao nao wanajipanga jinsi ya kuwashawishi wanananchi wawaelewe na wawachague tena waliokuwa wabunge wao.
Naomba nitumie maneno ya busara na mazito ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ambayo yanaweza kutumiwa na CCM kujaribu kupangua hoja hizo mbele ya wananchi, na hoja hizi zikachuliwa kama lawama za kawaida za kisiasa mbele ya wananchi ambao wengi wao hufuata mapenzi ya vyama vyao kabla hawajafikiria kuhusu mtu aliyepewa ridhaa.
Kuhusu usaliti, ni dhahiri kuwa usaliti unaozungumziwa kwenye siasa ya Tanzania ulipata umaarufu zaidi kwenye uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 ambapo ni CCM ambao walikuwa wanawatuhumu baadhi ya viongozi au wagombea kuwa ni wasaliti kwa kusaidia kambi ya Ukawa.
Alipoulizwa Mbowe kwanini amempokea Mheshimiwa Edward Lowassa na kumpa kugombea, alijibu kuwa “mtaji wa chama cha siasa ni watu.” Jibu hili linaweza kutumika pia na CCM kwani nao wanauhitaji mtaji huu hasa Bungeni kwa kucheza karata za kisiasa.
Pia, watu hao sasa ni wasaliti kwa Chadema lakini ni chachu ya ushindi kwa CCM wakijaribu karata yao ya kuyarejesha majimbo waliyoyapoteza mwaka 2015.
Kuhusu gharama za uchaguzi kuwa mzigo kwa wananchi, CCM wanaweza kuicheza pia karata hiyo kwa kutumia maneno ambayo hutumiwa sana na wapinzani kuwa ‘demokrasia ni gharama’.
Gharama hizi za uchaguzi mdogo zimetokana na kuwepo kwa fursa hiyo katika demokrasia. Zinaweza kuwa zinaumiza sana au zinaudhi, lakini zisingeweza kuwepo kama demokrasia isingetoa nafasi ya mtu kuhama na kujiunga na chama chochote, na fursa ya sheria kuhusu uchaguzi husika. Na ukiwaza gharama utaweza kutaka hata chaguzi zisiwepo kwani kweli zinatumia fedha nyingi, lakini hii haiwezekani kwenye nchi ya kidemokrasia.
Hizi ni sarakasi za siasa ambazo hatukuwahi kuzishuhudia ambazo siku zote mzigo wa gharama humuangukia mwananchi lakini kila chama kinatumia fursa hii ili kuhakikisha kinanyoosha nchi kwa sera na watu kinaowaamini.
Chadema ambao wameweka wapinzani makini na bila shaka wanauzika kwenye majimbo husika wakipambana vikali na wale ambao tayari walikuwa wameshauzika miaka miwili iliyopita, wanapaswa kujikita katika kutafuta hoja za kuwanadi wagombea wao zaidi ili kuzivuka hoja hizi za awali.
Wanapaswa kutotumia muda mwingi kuzungumzia ‘wakati huu hatukubali’ na badala yake wajikite zaidi kwenye ‘vita kamili ya hoja’ na sio vinginevyo.
Kujiamini kwao kuendane na nguvu kubwa ya hoja ya kuwanadi wagombea wao ambao ni wapya katika maeneo husika ili mwisho wasije wakamlaumu ‘refa’ kama matokeo ya mchezo hayatakuwa kama walivyotarajia.
Hizi ni chaguzi nzito na zenye ushindani mkubwa sana kwani tayari kila chama kimewatoa majembe wake kwa ajili ya kujinadi. Kwa upande wa Chadema, Mwenyekiti wake Freeman Mbowe ameanzisha na majembe yake huku Edward Lowassa ambaye ana ushawishi mkubwa kwa wananchi ndani ya chama hicho anahusika pia.
Kwa upande wa CCM, Dkt. Mwigulu Nchemba jana alianzisha na leo anaendelea akiwa na majembe ya chama hicho.
Tukubali wote kuwa hii ni mechi ngumu ya kisiasa na lolote linaweza kutokea. Chadema na CCM wote wana nafasi sawa ya kumshawishi mpiga kura aweke vema kwa mgombea wao.
Mwisho, kila chama ni vyema kikaweka mawakala waaminifu na wawe na barua za utambulisho mapema kabisa ili kuepuka usumbufu, kulaumiana na kuweka mazingira tata.
Ni vyema kila chama kifanye kazi yake ipasavyo ili kuepuka kuvitupia lawama vyombo vingine kama Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jeshi la Polisi na Wasimamizi wa kura.
Yote kwa yote, amani ya Taifa letu kwanza. Tupambane kwa hoja na tuepuke mambo yatakayoivunja amani yetu. Haki itawale pande zote na uchaguzi uwe huru na haki. Natamani kuona mshindi akipongezwa na mpinzani wake kama ilivyo kwa baadhi ya nchi zilizokomaa kidemokrasia.