Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema kuwa katika uchaguzi mdogo wa madiwani utakaofanyika Novemba 26, 2017 katika kata 43 utagharimu kiasi cha Sh bilioni 2.5.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Kailima Ramadhani, ambapo amesema kuwa msingi wa bajeti ya uchaguzi unategemea idadi ya vituo vya kupigia kura na idadi ya wapiga kura walioandikishwa katika kata husika.

Amesema idadi ya Wapiga Kura ndio inatoa bajeti ya mahitaji ya vifaa vya kuendeshea uchaguzi kama karatasi za kura pamoja na idadi ya vituo ambavyo vinakuwa na watumishi wasiopungua wanne. Kailima alitoa mfano kwamba Kata yenye vituo 41 ina bajeti kubwa kuliko Kata yenye vituo vikubwa.

Aidha, amesema kuwa katika kituo cha kupigia kura kina watendaji wanne ambao ni Msimamizi na Msimamizi Msaidizi, karani mwongozaji na mlinzi wa kituo “lakini pia kuna watu wa ziada kama Wasimamizi Wasaidizi wako ngazi ya kata na jimbo ambao wanahusika kusimamia zoezi la Uchaguzi katika maeneo husika.

“Kwenye uchaguzi huu mdogo bajeti yetu ni Sh. bilioni 2.5. Sio kwamba kila Kata itatumia gharama sawa za fedha hizi, bali kuna kata itatumia milioni 20 kutokana na idadi ya vituo vya kupigia kura kuwa vichache na kata yenye vituo vingi kwenye uchaguzi huo itatumia Sh milioni 150,” amesema Kailima.

Vile vile Tume pia imeviasa Vyama vya Siasa vinavyohusika kwenye uchaguzi mdogo wa madiwani kutekeleza maadili ya uchaguzi ya 2015 waliyokubaliana kuyafuata na ameonya kuwa chama au mgombea atakayekika maadili hayo atachukuliwa hatua kama ilivyoanishwa kwenye maadili hayo ya uchaguzi.

Hata hivyo, Mkurugenzi huyo ameongeza kuwa Vyama vya Siasa vinatakiwa kuhakikisha vinawaelemisha wafuasi,Wapenzi na Wananchama wao juu ya kutekeleza maadili hayo katika kipindi chote cha kampeni. Alisisitiza kuwa iwapo wafuasi wa vyama vya siasa watakikua maadili hayo, chama husika pamoja na mgombea wake watachukuliwa hatua za kinidhamu.

 

TFF kuzilipa timu ASFC mapema
Nyalandu: kilichobaki kwa sasa ni kuimarisha Demokrasia