Wananchi nchini Burundi wanafanya uchaguzi kuandika historia mpya katika safari ya democrasia leo Mei 20 baada ya Pierre Nkurunziza kuwaongoza kwa mika 15.
Ingawa wapo wagombea saba wanaowania kurithi kiti cha Rais Nkurunziza anayeondoka madarakani, mgombea wa chama tawala CNDD/FDD Evariste Ndayishimiye na Agathon Rwasa wa chama cha CNL ndio washindani wakuu.
Mkuu wa Tume ya Uchaguzi, Pierre Claver Kazihise, mapema Mei 17 wakati wa kampeni aliwaonya vikali wale wote watakaokwenda kinyume na sheria, huku waziri wa afya akiwakumbusha wagombea na raia kuzingatia kanuni za kuepukana na ugonjwa wa COVID-19.
Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), imesema haitapeleka waangalizi wake kutokana na masharti yaliyotolewa na Serikali ya nchi hiyo kuwa waangalizi watatakiwa kukaa karantini siku 14 ambazo zitamalizika wakati uchaguzi huo umeshafanyika.
Wachambuzi wa masuala ya siasa, kijamii na kidiplomasia, wameshauri Serikali mpya itakayochaguliwa kuandaa mjadala wa Kitaifa ili kubaini matatizo na changamoto za wananchi na kuzifanyia kazi.