Na Josefly
Leo, imekuwa siku njema kwangu kumsikiliza tena Darassa yule wa ‘Muziki Gani’. Nikatulia nikatumia dakika zangu 3 na sekunde 43 kusikiliza pini jipya kutoka kwake akiwa na Jux, lililobatizwa jina la ‘Leo’. Baada ya hapo nilirudia mara nne.
Nimevutiwa kuandika kitu kuhusu wimbo huu kwa sababu kwangu nahisi ndio wimbo wangu wa pili mkubwa kutoka kwa Darassa baada ya kombora la ‘Muziki Gani’. Najua aliwahi kutoa ngoma nyingi kali baada ya ‘Muziki Gani’ lakini sikio langu halikuguswa kama alivyoligusa na ‘Leo’, na jinsi alivyoweza kuendana na Jux (chemistry).
Darassa ametulia tena kwenye hii ngoma, ameandika mashairi rahisi kushikika lakini yenye ubunifu, yanayoacha tafakuri kwenye kichwa cha msikilizaji ambaye wakati huohuo amewekwa kwenye picha ya kuwa ‘batani’.
Mwanzo tu wa wimbo huu unavuta usikivu wa haraka sana. Darassa anakiri kuwa amechelewa na aliwekwa kwenye foleni. Hili limenipa tafakuri ya haraka, ni kweli Darassa anajua hakuwahi kuwapa mashabiki wimbo wa burudani kama ‘Muziki Gani’ na amekuwa akiwekwa kwenye foleni na nyimbo nyingi kali za wasanii wengine kwenye upande huo. Ni dhahiri sasa anaamini ‘Leo’ itamrudishia heshima yake ya ‘Mr. Burudani’ na kumuweka mbele ya foleni.
“Hello, it’s me again, Mr. Burudani take away the pain/Pole kwa kuchelewa, si unajua foleni…” Darassa amefungua ngoma yake.
Mkali huyu ambaye zamani alikuwa akifahamika kama ‘Mr. Sikati Tamaa’ na sasa ni ‘Mr. Burudani’, kwa lugha ya mtaani tunaweza kusema ameshinda sana kwenye verse (ubeti) ya ufunguzi, lakini ameua zaidi verse ya pili.
Ni ngoma ambayo mlengo wake ni kuzungumzia kinachoendelea kwenye eneo la starehe, lakini imekuwa na maneno mengi yanayoburudisha ubongo zaidi na kuufanya utafakari.
“Umebugi step hebu chekicheki, if I’m not mistaken umegeuza gazeti/ Ukitaka kazi ya jeshi don’t forget hakuna wa kukupetipeti,” anarap.
Neno ‘umegueza gazeti’ linaweza kutafsiriwa kwa maana nyingi, lakini maana mojawapo inaweza kuwa unajaribu kumsoma Darassa haumuelewi kwa sababu taswira unayomtengenezea sio yeye alivyo, ni kama umegeuza gazeti, hautamuelewa.
Kingine nilichokipenda ni kile kitu ambacho Jux amefanya kwenye huu wimbo, ingawa mistari ya mashairi ya chorus (kibwagizo) yanayonekana kuungwa kimtindo, lakini ufundi wa melody alioutumia kuviunga vifungo vya maneno ya chorus hiyo umeing’arisha zaidi.
Kwa kupita vizuri kwenye nyimbo za wasanii wa rap/hip-hop, Jux amenithibitishia jambo kubwa kwenye wimbo huu, kuwa yeye ni mkali kweli wa RnB. Kama alivyoua kwenye ‘Hatufanani’, humu ndani pia ameua vizuri sana Bwana Juma Jux. Kwa wenzetu wa Marekani ambapo muziki wa rap umekita mizizi na sisi tunafuata, wanampima zaidi pia msanii wa RnB anapokaa katikati ya michano. Kama unakumbuka ‘I need a Girl’ ya Diddy, chorus (kibwagizo) ya kwanza ilifanywa na Usher Raymond, na Remix ikafanywa na Ginuwine. Uliibuka mjadala wa nani ameua zaidi hiyo chorus, lakini ukweli ni kwamba kila mmoja alifanya kazi yake ipasavyo.
‘Chemistry’ yao imeonekana zaidi pale walipokuwa wakipokezana kwenye verse. Jux amechombeza vizuri sana na Darassa amedaka vichombezo hivyo na kuendelea kufanya kile kinachomfanya aitwe ‘Mr. Burudani’.
Ingawa najua kuna wengi ambao wamewahi kueleza kuwa mtindo anaoenda nao Darassa utachosha, nadhani kwenye hii ‘Leo’ watavumilia hadi mwisho na watairudia.
Mpishi wa wimbo huu, Abbah amefanikiwa pia kwenye mdundo, kinanda chenye tone kali kinachousindikiza mdundo mkavu mwanzo kidogo, kisha kuimba na Jux kwenye chorus kimetengeneza melody nyingine ambayo itawainua wengi kwenye kiti hasa kwenye kumbi za starehe na kumbi za usiku (night clubs).
Naomba nisizungumzie sana kazi ya Hanscana, muongozaji wa video ya ‘Leo’. Kwa ufupi ameitendea haki, lakini wingi wa wanawake wenye mitetemo ya pwani kunaweza kuzua mengi… lakini pia kuvuta macho hasa ya wanaume kutulia kwenye vioo vya runinga, simu janja au kompyuta kujionea uumbaji!
Video ‘imechangamka’, maeneo yametengenezwa vizuri na washiriki wote wamefanya kazi inayotakiwa kweli, wamekuwa active kwenye kila nukta.
Video ya ngoma hii imeanza vizuri, kwani ndani ya saa mbili tangu aiweke YouTube ilivuta views zaidi ya 29,000. Kwa wasanii wengi wa rapa/hiphop views huwa ni changamoto, lakini hili linaonekana kutomhusu Darassa kwenye ‘Leo’.
Kwa mtazamo wangu, ‘Leo’ itabaki kuwa juu; na huenda ikaanza kufuata nyayo za ‘Hatufanani’ ya Shetta akiwashirikisha Mr. Blue na Jux. Huu ni wimbo utakaomtoa Darassa kwenye foleni, ni moto wa gesi.
Kama anavyosema mwenyewe, “kama ulijua cheche, imekuwa kasheshe huwezi kuzuia mvua acha inyeshe/ Utauawa bure sijalala nimeficha tu makucha.”
Changamoto kwenye wimbo huu, kwanza ni maneno ya kwenye chorus ambayo baadhi ya waandishi wataona kama hakuna muunganiko kati ya buti kuchanika na spika kukita. Ni kama vilitafutwa vina zaidi ya maana, ili mradi chorus iwe rahisi kukaririka.
Pili, uimbaji wa Darassa ni kama uleule na unaweza kudhani labda ni midundo tu na mashairi vinavyotofautisha kati ya wimbo mmoja na mwingine. Lakini kwenye hili, naweza kumtetea kuwa yeye haimbi, anarap kwa mtindo mpya (Lakini ukimwambia Nash MC kuwa Darassa amerap humu anaweza kukuchapa makofi,lol). Huo ndio mtindo wake wa kurap, anacheza na vituo na mirindimo tu!
Ni vigumu kwa wale rapas wakali kama Nash MC, Nikki Mbishi, Wakazi na wengine kukubali kuwa anachofanya Darassa ni kurap tena usije kutaja hiphop, ni kama Eminem ambavyo anawaponda wenye mitindo kama ya Migos kuwa ni ‘Mumble rapers’, lakini bado wanashinda tuzo za kwenye vipengele vya rap.
Darassa wamefanikiwa pia kuunganisha mashabiki wao, wale warembo wa Jux na wale akina ‘Mr. Sikati tamaa hadi Mr. Burudani’.
Haya, tuendelee tuenjoy na ‘Leo’, na toa maoni yako kama ni moto wa gesi kweli au kifuu?