Tanasha Donna, Mkenya ambaye naamini wengi hasa Watanzania walimfahamu baada ya kutambulishwa kuwa ni shemeji yao mpya kwa Diamond aka Simba, juzi aliachia video ya ngoma yake mpya ‘Radio’ ambayo imepata mapokezi ya aina tofauti-tofauti.
Baada ya kuangalia video ya wimbo huo, kwanza nilikumbuka msemo wa mtangazaji mmoja wa Radio aliwahi kuniambia siku moja kuhusu uhusiano wa Tanasha na Diamond kuwa “Simba hali nje ya pori, akila nje ya pori ujue ataacha vilio…” Pori alimaanisha uwanja wa sanaa. Wengi alikuwa nao Diamond ni wasanii iwe wameficha makucha ya sanaa au wameyaachia. Sasa nawe tafsiri unavyoweza.
Kama ulikuwa haufahamu, huu sio wimbo wa kwanza wa Tanasha, labda ni wimbo wa kwanza tangu awe ubavuni mwa Diamond. Sauti yake imewahi kupenya na amekuwa miongoni mwa ‘wahangaikaji wanaosaka tobo’. Kwahiyo ‘Radio’ ni muendelezo wa msako wa tobo la kutokea kwenye ulimwengu wa muziki, na kwa bahati nzuri, hivi sasa amefanikiwa kulishika jicho la mamilioni ya mashabiki wa Diamond na yuko kwenye spotlight. Mwaka jana tu alishirikishwa na Nviiri kwenye ngoma waliyoiita ‘Ex Anaiva’.
Kama unamuona kwa mara ya kwanza Tanasha kwenye video ya wimbo wake, utakubaliana na mimi kuwa ni tofauti sana na yule uliyekuwa unamjengea picha akiwa pembeni ya Diamond aka Chibu. Yule mwenye sura ya upole ameazima ukaksi wa Cardi B.
Tanasha ameanza kutenda haki juu ya mdundo akiwa studio. Uandishi wa mashairi unadhihirisha kuwa ulifanywa na msanii anayejielewa. Ni wimbo wa tambo na majigambo ambao hakika umeandikwa vizuri. Binafsi nimependa pia jinsi alivyopita na mtiririko wa kuimba wenye harufu ya miondoko ya rap ya kisasa.
Sauti ya Tanasha ni ya ndege tetere inayofaa, inapenya kiurahisi. Hivyo, kama mashairi na flow ziko vizuri basi inamalizia tu kufunga magoli.
Naamini uandishi huo umeguswa kwa namna moja au nyingine na rapa Barak Jacuzzi, Mkenya aliyekulia nchini Marekani ambaye ameshirikishwa kwenye wimbo huo. Michano ya rapa huyo kwenye wimbo huu imeboresha na kuufanya kuwa mfupi. Kumekuwa na ‘chemistry’ ya aina yake. Kwa wasio mfahamu Barak Jucuzzi, sio msanii mpya, albam yake ‘The Juice Bar2’ ilionesha uwezo alionao.
Kwa uhalisia, katika uimbaji, sio kwamba kwa sasa Tanasha ni msanii mwenye kiwango cha uwezo wa Vanessa, Nandy Ruby, Size 8 bali ni mwimbaji mwenye kipaji cha kiwango kinachoridhisha.
Video ya ngoma hii iliyoongozwa na Ivan Oddie ninaipa alama za juu zaidi ya audio. Tanasha amefanya kazi nzuri kama msanii, wengi watamfananisha na Cardi B pamoja na Aaliyah jinsi alivyojaribu kufanya yake. Amejua kucheza na kamera kwenye kila shot aliyotokea. Sifa za kipekee kwa aliyemchagulia mavazi, make-up na aliyemfunza kucheza kwa ajili ya video (choreographer).
Video ina kiwango kizuri, imeandikiwa script inayoanzia kwenye studio ya Radio kuweka umaana wa ‘Radio’. Mbali na uzuri wake, kuna vitu vingi vitakavyonasa jicho lako, kuanzia mtangazaji anapotambulisha wimbo halafu inaonekana kuna mkono unaweka kanda kwenye radio na sio CD/Santuri.
Kwa jinsi alivyojiweka kwenye video, ukimkumbuka Tanasha yule cha upole hivi, utairudia tena. Changamoto ni kwamba kwa wale mashabiki wa nyimbo za Diamond, huu unaweza ukawa sio wimbo wenye mlengo wao hata kidogo, yaani wengi hawatauelewa kabisa.
‘Radio’ imeshaangaliwa zaidi ya mara 124,000 ndani ya siku mbili na nusu. Hii sio takwimu ya kuvutia sana kwakuwa sio wimbo wa kuitwa ‘hit’ ila ni wimbo mzuri.
Huo ni mtazamo wangu, wewe pia unayo nafasi ya kutoa maoni yako, Tanasha huyu nyota wa video ya Ali Kiba ‘Ninagharamia’ na ubavu wa Diamond amepiga ndani kwenye nyavu au amepiga nje?