Na: Ghati

Ulimi wa mwenye kiu hulitamani tone moja la maji linalodondoka kutoka kwenye tawi, tamaa ambayo inaweza kugeuzwa kuwa furaha kuu kama utapata jagi lililojaa maji safi na salama. Hivi ndivyo naweza kufananisha kiu ya mashabiki wa Ali Kiba ilivyokuwa juu ya wimbo wake mpya. Je, alichowapa ni tone la maji, amewavuruga au amekata kiu yao?

Takribani saa 24 zilizopita, Ali Kiba alivunja ukimya wa muda mrefu kwa kuachia wimbo wake mpya alioupa jina la ‘Seduce Me’. Wimbo ambao ulisambaa kwa haraka na kupata mafanikio makubwa kwenye mtandao wa YouTube ambapo hadi naandika uchambuzi huu umeangaliwa zaidi ya mara 610,400. Ni mafanikio makubwa sana kwa upande huo.

Nilipousikiliza kwa mara ya kwanza ‘Seduce Me’, kilichonijia kichwani ni ‘Ali Kiba amekuja kivingine kabisa’. Nikaanza kufikiria misemo ile ‘iliyopendwa’ na wahenga unapotaka umati umhukumu mtu aliyejaribu kuushawishi kumkubali, unauliza ni ‘Hai au Hoi?’

Melodi:

Kwanza nianze na melodi ya ‘Seduce Me’ na jinsi ambavyo sauti ya Ali Kiba imesikika kwenye wimbo huu. Kwenye hii sekta Ali ameendelea kusimamia sifa aliyowahi kupewa na Mfalme wa RnB duniani, R.Kelly kuwa yeye ndiye aliyekuwa mwimbaji mwenye sauti bora zaidi katika mradi wa One8 (Best Vocalist). Ali anasikika akiwa kwenye ubora wa sauti ambazo hazikuchezewa na ‘outo-tune’ au kubanwa. Kwa ufupi, melodi na sauti ni kubwa kama Ali Kiba.

Ushairi:

Kwa upande wa mashairi, nianze kwa kueleza kile nilichokielewa. Ali ameamua kufanya kiitikio kwa lugha ya Kiingereza na kuitumia pia lugha hiyo kwenye kibwagizo na baadhi ya maneno, hivyo kufifisha matumizi ya Kiswahili kwenye wimbo wake tofauti na nyimbo nyingi tulizowahi kumsikia. Hii inanifanya nichelee kusema wimbo huu huenda umelenga zaidi soko la Kimataifa na mashabiki wenye uwezo wa kati au uwezo wa juu hapa kwetu. Wengine wataupenda kadiri watakavyouelewa kwani muziki ni lugha ya dunia (universal language). Kuanzia jina tu la wimbo, wengi ‘tuta-Google’ au kuzitafuta kamusi zetu. Japo inaweza isiwe sababu ya msingi kwani nyimbo za Nigeria hupenya Tanzania na lugha ngumu kumeza hivyohivyo.

Pacquiao aungana na ‘Timu Mayweather’, amshusha McGregor

Kwa tafsiri ya mtu kama mimi ambaye nakifahamu kiingereza kwa hisani ya watu wa…, Ali Kiba anamtaka mrembo ‘amtongoze’ au kwa lugha ya kisasa zaidi ‘amtege’ kwa namna ambayo sio ya kawaida. Lakini anamtahadharisha kuwa yeye sio mwanaume wa kutulia na mwanawake.

“Nakuona unakata, be careful sister (kuwa makini dada), na kama unataka… they call me heartbreaker,” Ali Kiba anaimba huku akimuweka wazi msichana huyo kuwa ana majina mengi aliyopewa na wanawake ambao ameshawavunja moyo. Kwenye ubeti wa pili, Ali anampa moyo mrembo huyo kuwa pamoja na kuwa ‘Kipusa mpasua Kichwa’ yuko vizuri kwenye kuhonga tena magari ya kifahari (mandinga).

‘Seduce Me’ naweza kusema ni wimbo ambao baadhi niliowasikia wanaamini hautashika kwa nguvu ya ‘Aje’ hata kama utaangaliwa mara nyingi zaidi, utakuwa wimbo utakaoshika taratibu lakini utakuwa na ‘wasikilizaji wake’ pia. Inaelezwa kuwa sio wimbo ambao utarushwa kwenye halaiki ya Watanzania utegemee kupokelewa kwa nguvu kubwa itakayozidi ‘Aje’. Lakini unaweza kuwa wimbo mkubwa zaidi kwenye maktaba ya nyimbo kubwa za mwaka huu na ukaishi maisha marefu zaidi ya nyimbo hizo. Inaweza kuwa kubwa zaidi pia ughaibuni.

Production (utayarishaji):

Ingawa mimi sio mtaalam wa utayarishaji wa muziki, nimeishi na rafiki zangu ambao ni watayarishaji wakubwa wa muziki na wamekuwa wakinisikilizisha nyimbo zao na mimi nikawa natoa ushauri ambao walikuwa wanauzingatia pia kwenye mambo yao, kama msikilizaji mzuri.

Nilipousikia wimbo huu, nilisikia kama kuna mambo fulani hayako sawa kwenye upande huo. Nilihisi wimbo uko chini, kama haujafunguka. Yaani ile sauti tamu ya Mfalme Kiba kama siipati vizuri ikiwa imeachiwa kama ilivyokuwa kwenye ‘Aje’. Naitaja sana ‘Aje’ kwani ndiyo wimbo wa mwisho wa Kiba, hivyo ni rahisi zaidi kuukumbuka.

Lakini nimemsikia mtayarishaji wa muziki, Dupe akiuzungumzia wimbo huu kwenye YouTube channel ya Simulizi na Sauti (SnS). Amesema ni kweli utayarishaji wake una kasoro hiyo.

“Kama tunaita kwamba hili ni soko la ushindani, kwenye audio production huu wimbo uko chini. Ukiangalia kwenye instruments (upigaji vyombo) na nini, lakini uimbaji ni hatari,” alisema Dupe akiungwa mkono na Skywalker.

‘Seduce Me’ tayari ni wimbo mkubwa na umefanya vizuri. Kilichobaki sasa ni kupima ukubwa wake, yaani ni mkubwa kiasi gani na kama ukubwa wake unazidi zile kubwa alizowahi kuzitoa. Hadi sasa iko katika nafasi ya kwanza kwenye Trending YouTube na imeng’ang’ania hapo kwa zaidi ya saa 20 huku waangaliaji wakiendelea kumiminika.

Ingawa ametoa video, leo naomba nisiiguse video yake, tutaichambua siku nyingine hapa hapa Dar24.

Nakuachia uwe mmoja kati ya majaji kwenye hii halaiki ya Wapenda Muziki Mzuri. Je, ‘Seduce Me’ ni Hai au Hoi?
Tujikumbushe Aje:

Matonya awavaa WCB, adai wamemuibia ‘Zilipendwa’
Video: Diamond, Rayvanny, Harmonize, Rich Mavoko kwenye 'Zilipendwa', Itazame hapa