Je ni ukoko wa LIBIDO DOMINANDI kutoka kwa watawala wa Kenya.?

Na Dr. Bravious Kahyoza,PhD.

Wiki moja iliyopita, Prof. Issa Shivji akihojiwa na John Githongo kwenye Elephant TV(Kenya), mawasilisho yake yalichukuliwa na hoja yake kuu ya “Katiba hazitengenezi Mapinduzi,Mapinduzi hutengeneza Katiba”.

 Katika kile kinachoakisi maoni ya kisomi ya Prof.Shivji; 20/9/2020, Jaji Mkuu wa Kenya ametoa ushauri(wa lazima kufuatwa) kwa rais wa nchi hiyo, Ndg.Uhuru Kenyatta kuvunja Bunge kwa sababu ya bunge hilo kushindwa kutunga sheria ya kuruhusu kanuni ya theluthi mbili kwa wanaume na wanawake kwenye vyombo vya maamuzi nchini humo maarufu kama ” Two Third Gender Rule”.

Sheria hii haikuwezekana nje ya sababu za kisheria zinazotajwa sana; lakini juu ya yote ni hulka ya LIBIDO DOMINANDI ya kundi moja kutaka muda muda wote kutawala wengine; kwa muktadha wa Kenya, Libido Domindi ya serikali dhidi ya mihimili mingine na Libido Domindi ya wanaume dhidi ya wanawake. Siyo nia yangu kueleza hayo sana; ni lengo langu kuonesha yanayoweza kujiri kuanzia kesho

WAMEFIKAJE WALIPO?

Ushauri wa Jaji David Maraga umefikiwa baada ya maombi sita(6) ya kulitaka Bunge kutimiza takwa la hilo la  Kikatiba kati ya 12/April/2019 na 20/July/2020 kugonga mwamba. Kwa mujibu wa katiba ya Kenya Ibara ya 27(3), 81 na 100 zinataka kuwepo kwa uwiano huo wa kijinsia kiuchumi, kisiasa, kijamii na kitamaduni ili wanaume na wanawake wawe na usawa, uhuru na wasibaguliwe kwa jinsia zao.

Pamoja na amri 4(nne) za kulitaka Bunge kuweka sheria hiyo, hakuna hatua zilizochukuliwa.

UAMUZI WA JAJI MARAGA UNA UZITO KIASI GANI?

Kwanza, uamuzi huu umefikiwa baada ya mahitaji ya kutekeleza katiba kukiukwa. Kwa mujibu wa njia thabiti za kutekeleza katiba ya mwaka 2010; Bunge linatakiwa kutunga sheria  48 katika kipindi cha miaka 5(tano) toka siku katika mpya ilivyozinduliwa rasmi(yaani kutoka August 2010 hadi August 2015). Hadi wakati huo, Bunge liliweza kufanya sheria 47 na kubakiza hiyo moja(maarufu kama 2/3 Gender Rule). Miaka 9(tisa) baadae bado sheria hii haijatungwa.

Kwa sababu hiyo, Ibara ya 261 inahusika. Kwa mujibu wa Ibara hii, mtu yeyote anaweza kupeleka maombi kwa Jaji Mkuu kumtaka kushauri rais avunje bunge, na Jaji Mkuu atalazimika kumshauri rais, na rais atalazimika kutekeleza ushauri huo. Watu watano na Jumuiya ya Wanasheria wa Kenya walifanya hivyo kwa Jaji Mkuu na Jaji Mkuu amefanya aliyofanya kwa kumshauri rais.

YAPI YANAWEZA KUJIRI.

Mosi, kuna uwezekano mkubwa wa wakubwa kutaka kuchelewesha mambo. Hii ni kwa sababu ya LIBIDO DOMINANDI kwenye siasa za Kenya. Rais  Uhuru Kenyatta anaweza kujaribu kufanya yafuatayo.

A. Anaweza kusema hajapata ushauri huo na anasikia tu ili ajipange.

B. Kwa sababu kuna utaratibu wa Gazzete Notice kabla ya uchaguzi mwingine, anaweza kutumia muda huo kucheza danadana.

C. Spika anaweza kutumia muda mwingi kwa kisingizio kuwa bado anawapa taarifa wabunge.

Pili, kwa kutumia Ibara 102(1) ambayo inasema muhula wa bunge unaisha siku ya tarehe ya uchaguzi mwingine.

Ibara ya 136(2)(a) inayosema kuwa uchaguzi wa Rais utafanyika tarehe ileile ya uchaguzi wa wabunge ambayo ni Jumanne ya pili kila baada ya miaka 5 toka uchaguzi ulioisha.Kwamba wale wabunge 337 ambao ni wabunge wakuchaguliwa, wawakikishi wa  wanawake na maseneta wanachaguliwa pamoja na rais.

Na kwa sababu ya Ibara hizo hapo juu, maswali makubwa yatakuwa;

Je uchaguzi mwingine utawahusu wote wabunge, rais, magavana na MCA?

Je miaka 5 inatahesabika kutoka 2017 uchaguzi ule ulipoisha au toka 2020 ikiwa uchaguzi umefanyika?

Kwa sababu katiba haisemi kipimo cha moja kwa moja cha urefu kwa kukaa madarakani kwa rais badala yake inahusisha muda wa kuchaguliwa bunge na uke muda rais, Je muda wa rais utakuwa hadi 2022 au 2025 ikiwa uchaguzi mpya utafanyika 2020?

Je, utakuwa muendelezo wa LIbido Dominandi?

Mambo matatu yaweza kutokea kwa maoni yangu.

A. Bunge linaweza kuchaguliwa upya 2020-2025, lakini muda wa rais ukatofautishwa na wa bunge, kwa hiyo rais akaondoka mwaka 2022. Hii ni kwa sababu katiba pia haisemi ikiwa waondoke kwa pamoja(simultaneously)

Shida hapa ni kuwa unaweza kuwa na rais mpya na bunge la kale. Hii ni dhahama.

B. Bunge jipya litachaguliwa, rais atachaguliwa 2020 na hivyo kwa sababu katiba inasema uchaguzi ufanyike siku moja, basi rais na wabunge watatoka 2025.

Shida hapa ni kuwa Katiba itakuwa imebadilishwa bila hata referendum.

Lakini ikiwa itakuwa hivyo, na bunge lisiifanye hiyo 2/3 gender  rule, Uhuru na bunge wataendelea hadi milele? Prof Shivji anasema Katiba hazitengenezi Mapinduzi, Mapinduzi hutengeneza Katiba.

C. Au bunge litachaguliwa tena, rais atachaguliwa tena na kwa kuwa Ibara ya 142 inasema ni vipindi viwili vya miaka mitano mitano, na rais Kenyatta kashatumikia karibu nusu ya muhula wa pili, basi amalizie muda uliobaki na aende nyumbani 2022.

Shida ya hapa ni kama niliyoeleza kwa matarajio (A).

NA UCHUMI JE?

Kati ya August/2017 na November/2017 kwa siku 126, uchumi wa Kenya ulipoteza takribani Shilling za Kenya Trillion 1 au Billion 1 kwa kila saa ya kazi.(kwa kutumia takwimu za Hazina)

Mwaka mmoja kabla ya uchaguzi na mwaka mmoja baada ya uchaguzi, uchumi wa Kenya kwa maana ya pato ghafi husinyaa kati ya 1.2%-2% kwa kila mzunguko wa uchaguzi toka 1992, hii athari ya Maraga(Maraga Effect) itaufanyaje uchumi ulipigika kwa Covid 19 na ufisadi uliokithiri?

Mchumi mashuhuri zaidi kwa ukanda wa Afrika kwa sasa(David Ndi) na wenzake wamekwenda mahakamani kupinga sindimba za BBI kwa hoja ya Basic Structure Doctrine. Ukimsikiliza Dr.Ndi toka sarakasi hizi zianze kwenye kitovu cha hoja zake ni uchumi ulioratibiwa vibaya; nyundo ya Maraga inampa hoja zaidi Dr.Ndi.

ATHARI YA MARAGA(MARAGA EFFECT).

Kuna watakaosema; kwa nini Maraga hakufanya hivi 2016 au 2018 au 2019? 

Nafikri Maraga alikuwa naye anaotafuta pale panaoikaba vizuri Libido Dominandi ya watawala.

Hata hivyo, athari ya Maraga inaweza kuhitimishwa na mambo makuu 3.

A. Kufuta uchaguzi 2017

B. Kuvunja Bunge 2020

C. Unaweza kumfurusha rais Uhuru Kenyatta kabla ya muda wake kufika 2022.

Uamuzi wa Jaji David Maraga umefungulia songombingo za siasa kati ya Uhuru na Ruto katika uwanja mpya kabisa.

Selfie za kifo: Aanguka nje ya dirisha la gari likiwa kasi akijirekodi video
Kocha Sven aitangazia vita Gwambina FC

Comments

comments