Kocha wa zamani wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Patrick Aussems anatajwa kuwa miongoni mwa makocha wanaofikiriwa na Uongozi wa Young Africans, ambao unapambana kumsaka mrithi wa kudumu wa Cedric Kaze.

Aussems maarufu kwa jina la ‘UCHEBE’ kwa sasa yupo nchini Kenya anakinoa kikosi cha AFC Leopards hivyo ikiwa Young Africans watakuwa kwenye hesabu za kumpata itawalazimu kuvunja mkataba wake ndani ya kikosi hicho.

Mwenyekiti wa Klabu ya Young Africans, Mshindo Mbette Msolla amesema kwa sasa wameanza mchakato wa kumtafuta mrithi wa Kaze na wanaamini kwamba watampata hivi karibuni.

Masolla amesema wakati wakifanya mchakato huo, kikosi cha Young Africans kitakua chini ya kocha mzawa Juma Mwambusi hadi mwishoni mwa msimu huu.

Hata hivyo taarifa za kocha Aussems kutajwa ndani ya Young Africans bado ni tetesi, na hakuna kiongozi yoyote alieamua kujivika mabomu kwa kuweka wazi ukweli wa ushawishi wa kocha huyo kutoka nchini Ubelgiji.

Kocha Cedric Kaze aliyekuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo baada ya kuongoza kwenye michezo 18 ya ligi akishinda 10, sare 7 na kupoteza mmoja amechimbishwa kikosi hapo Machi 7 kutokana na kile ambacho kimeelezwa kuwa mwendo mbovu wa timu hiyo.

Young Africans inaendelea kuongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na alama 50 baada ya kucheza jumla ya michezo 23.

NBS: Mfumuko wa bei umepungua
Gomez: Prisons itatusaidia kuipa presha Young Africans