Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), limesema matarajio ya ukuaji wa uchumi Duniani, yanazidi kukumbwa na kiza na yanakosa uhakika huku matumaini ya kujikwamua na hatari hiyo yakizidi kufifia kwa mwaka 2022.
Mkurugenzi wa Idara ya utafiti wa IMF, Pierre-Olivier Gourincha ameyasema hayo wakati akizungumza na Waandishi wa Habari katika Makao Makuu ya IMF jijini Washington DC nchini Marekani, na kueleza kuwa hali ya kiuchumi inazidi kuwa mbaya.
Amesema, “Ulimwengu hivi karibuni unaweza kushuhudia kudorora kunakopeleka uchumi wa kimataifa ukingoni ikiwa ni miaka miwili tu baada ya kushuhudia mdodoro wa mwisho.”
IMF, imetaja sababu kuu za kudorora kwa uchumi kuwa ni kupanda kwa mfumuko wa bei, kupanda kwa viwango vya riba, thamani ya juu ya dola ya kimarekani, athari za vita vya Ukraine na kushuka kwa ukuaji wa nchi ya China.
Mkuu huyu wa idara ya Utafiti amesema, kinachohitajika ni ushirikiano wa pande zote ili kupunguza hatari ya Dunia kugawanyika na kuimarisha ushirikiano kwa kuboresha matarajio ya kiuchumi na kupunguza hatari ya kugawanyika kijiografia.
Hata hivyo, IMF imesema mfumuko wa bei unaoendelea nchini Marekani na mataifa makubwa kiuchumi, yamesababisha Benki Kuu kuongeza viwango vya riba.
Wakati huo huo, kumeibuka hoja ya usalama wa dola ya Marekani kutokana na na masoko yanayoibukia, huku yakikabiliwa na mfumo wa bei na gharama za malipo kwa deni la kiujumla ikiongezeka.