Kuzinduliwa kwa programu ya kushughulikia masuala ya wanawake, (UN Women) ambayo itafanyika kwa miaka mitano ili kuongeza kasi ya uwezeshaji wa mradi wa uimarishaji uchumi wa wanawake wa Vijijini, kutasaidia kuleta maendeleo ya kiuchumi kwa mtu mmoja moja na Taifa zima kwa ujumla.

Wakizungumza hii leo Oktoba 18, 2022 kwa nyakati tofauti ya mjini Magharibi Zanzibar na Manyoni Singida, baadhi ya akika mama akiwemo Wandiga Moses na Arafa Said wamesema wana imani kuwa mradi huo utatekelezeka kama ilivyokusudiwa, na kwamba wapo tayari kuonesha ushirikiano kwa uaminifu ili kufanikisha malengo yaliyokusudiwa ambayo yatakuwa na faida kwao na nchi.

Oktoba 12, 2022, mashirika ya Umoja wa Mataifa likiwemo la Chakula na Kilimo (FAO), Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD), Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) walizindua programu hiyo wakilenga kuwawezesha wanawake wa Vijijini ili kuwaletea maendeleo.

Kupitia taarifa yake, Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO), ilieleza kuwa mradi huo unaofadhiliwa na nchi za Norway na Sweden, utakaogharimu dola za Marekani milioni 5, utawanufaisha zaidi ya wanawake 8,000 wa vijijini katika mikoa ya Singida, Dodoma na Zanzibar kwa kusaidia ustawi wao kupitia mnepo katika sekta ya kilimo.

FAO ilieleza kuwa, nchini Tanzania chakula kinazalishwa na wakulima wachache, huku wanawake wakichangia nguvu kazi kubwa na kupata asilimia 80 ya mapato ya kilimo cha kujikimu, na kwamba ukosefu wa usawa uliojikita katika mifumo dume na kanuni za kijamii huwazuia wanawake kupata huduma za ugani za kilimo, masoko, ardhi na huduma rasmi za kifedha.

Katika uzinduzi huo, Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi wa Zanzibar, Suleiman Masoud Makame alisema, “usawa wa kijinsia ni muhimu katika kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu na Tanzania inatambua hili na imepitisha sera zinazoendeleza usawa wa kijinsia na sisi kama serikali tunatambua na kuthamini ushirikiano unaoendelea wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania.”

Mgomo waanza nchi nzima kudai nyongeza ya mishahara
Utekelezaji wa malengo SDGs washika kasi