Katibu Mkuu Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Profesa Godius Kahyarara amesema, uchunguzi uliofanywa na Wizara kuhusu kuadimika kwa vinywaji baridi, ulibaini kuwa sababu ambazo zilikuwa zikitolewa ikiwemo ukosefu wa sukari viwandani na kupungua kwa makontena ya kubeba mizigo kwa meli hazikuwa za kweli.
Amesema Wizara imebaini licha ya makontena kuadimika bado mizigo ilikuwa inasafirishwa nje kwa kipindi hicho, Wizara ilibaini kuwa tani 25,000 za sukari ya viwandani ziliingia nchini.
“Wazalishaji wa vinywaji baridi walionesha kuwa changamoto ilikuwa ni kwa wasambazaji na si ya uzalishaji. Bidhaa nyingine ambazo bei yake imekuwa juu kuliko uhalisia ni za vifaa vya ujenzi ambapo baadhi ya maeneo ilifikia mfuko mmoja wa saruji kuuzwa kwa shilingi 25,000,” amesema.
Amesema kuwa utafiti huo pia ulibaini mafuta ya kupikia ya alizeti yanauzwa mpaka Sh 196,000 kwa ndoo ya lita 20 na sukari ni kati ya Sh2,800 hadi 3,000.
Profesa Kahyarara amesema bei hizo ziko juu ya wastani wa bei zinazotozwa katika nchi za Afrika Mashariki na kusini mwa Afrika na hazitafumbiwa macho.
“Wizara haitamuonea mtu wala kumnyamazia yeyote atakayebainika kutoza bei ambazo hazina uhalisia,” alisisitiza.
Amesema licha ya serikali kuwa tayari kulinda viwanda vya ndani pia inajukumu la kulinda maslahi ya walaji hasa wa kipato cha chini, na kuahidi kushirikiana na wadau wote katika biashara hususan suala la usimamizi wa soko.