WAKATI Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ikiendelea kufanya uchunguzi dhidi ya Shilingi bilioni 1 zilizotolewa mwaka jana na Rais John Magufuli kwa ajili ya kusaidia maandalizi ya mashindano ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Vijana chini ya Umri wa miaka 17 (AFCON U-17), uchunguzi wa awali umeonesha fedha hizo kutumika vibaya.
Uchunguzi huo ulianza kufanyika mwezi uliopita ikiwa ni siku chache baada ya kuwepo kwa taarifa zilizodai kuwa, Shirikisho la Soka hapa nchini (TFF) limekuwa na matumizi mabaya ya fedha hizo zilizotolewa na rais pamoja na zile zilizotolewa na wadau wengine wakiwemo NSSF kufanikisha mashindano hayo.
Licha ya fedha hizo kujatwa kuwa ni bilioni 1 lakini Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe amesema fedha ambazo zilitumika kufanikisha kila kitu katika mashindano hayo, bajeti yake ilikuwa ni zaidi ya bilioni 3.8 pamoja na ile iliyoingia kutoka katika vyanzo vingine kusaidia mashindano hayo.
Hadi sasa tayari viongozi mbalimbali wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) pamoja na baadhi ya viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) akiwemo Katibu Mkuu, Wilfred Kidao wameshahojiwa.
Kabla ya kumuhoji Kidao, Takukuru walikuwa wameshaanza kutipia nyaraka zote muhimu ambazo walizishapata ili kuambazo walizichukua kutoka kwa viongozi hao pamoja na Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo na Baraza la Michezo la Taifa ambao wanadaiwa fedha hizo kupita katika mikono yao.
Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Brigedia Jenerali John Mbungo wakati akihojiwa na kituo cha redio cha Wasafi, amesema kuwa, kwa sasa bado uchunguzi unaendelea lakini ule wa awali ukionesha matumizi mabaya ya fedha hizo.
Amesema, kwa sasa wanachokisubiri ni ripoti kamili itakayotolewa baada ya kumaliza kuwahoji viongozi wote ikiwemo wale wa Wizara pamoja na Rais wa TFF, Wallece Karia ambaye ameshaitwa Dodoma kwa ajili ya mahojiano baada ya Makao Mkuu ya ofisi za Takukuru kuhamishiwa jijini humo.
“Kwa sasa ni ngumu kusema nani ana hatia wala yupi hapa kwani uchunguzi bado tunaendelea kuwahoji na wachunguzi wanafanya kazi yao ili kuja na majumuisho. Lakini katika uchunguzi unakwenda vizuri na ule wa awali umebaini hakukuwa na matumizi sahihi ya fedha,” amesema Mkurugenzi huyo.
Amesema, watahakikisha kabla ya kutoa majibu watahakikisha wamewahoji watu wote hasa wale wa Wizarani ambao kwa namna moja au nyingine walihusika na fedha hizo.
Wakati Takukuru wakiendelea kuhoji viongozi hao, pia zoezi hilo litakwenda sambamba na kukagua nyaraka mbalimbali ambazo zinaonesha ripoti ya mapato na kila kilichokuwa kinatumiwa.