Waandishi wa Habari nchini, wametakiwa kuandika Habari za udhalilishaji na ukatili wa kijinsi kwa kuzingatia vigezo vyote vya kiuandishi, ili kuleta mabadiliko chanya katika jamii dhidi ya vitendo hivyo na kusaidia kujenga uelewa kwa jamii na taasisi zinazohusika kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Rai hiyo, imetolewa na Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari wanawake Tanzania, Zanzibar – TAMWA-ZNZ, Dkt. Mzuri Issa wakati akifungua Mkutano wa kuwasilisha ripoti za utafiti wa Habari za udhalilishaji kwa vyombo vya habari.
Amesema, Waandishi wa Habari wanatakiwa kuisaidia jamii kubadilika na kuwa na uwezo wa kuwalinda watoto na wanawake, ili kuona wanafikia ndoto zao huku akiiomba serikali kuweka utaratibu wa jamii kumlinda mtoto na Mwanamke dhidi ya vitendo vya udhalilishaji, ikiwemo kuweka sera na sheria ambazo zitaongeza nguvu ya kudhibiti vitendo hivyo.
“Licha ya kuwepo sera na sheria lakini hazijawabana watu kuogopa makundi hayo na badala yake wanaendeleza matukio ya udhalilishaji ipo haja ya kuwepo utaratibu maalum utakaowafanya wanaume kujiepusha na makosa ya udhalilishaji kwa kuepuka kuwadhalilisha watoto na wanawake,” amesema Dkt. Mzuri.
Awali, akiwasilisha ripoti ya utafiti huo mshauri elekezi wa utafiti wa masuala ya vitendo vya udhalilishaji, Dkt. Salum Suleiman Ali amesema utafiti umeonesha taarifa hizo zinaripotiwa lakini bado kuna mapungufu ya ubora wa Habari ikiwemo uchambuzi wa takwimu, uzingatiaji wa sera, sheria na mikataba ya kimataifa, mwendelezo wa habari na jinsi ya kuleta matokeo mazuri katika jamii.