Wizara ya Afya, imesema inapanga kuweka sheria na taratibu mbalimbali za afya kwa maeneo ya mipaka au yale yenye muingiliano mkubwa wa watu, ikiwemo kituo cha utoaji wa huduma kwa pamoja cha Rusumo mkoani Kagera, kinachounganisha nchi ya Tanzania na Rwanda.

Afisa Afya Mfawidhi wa Mpaka wa Rusumo, Oswad Kimasi amesema katika kukabiliana na magonjwa ya mlipuko ikiwemo Ebola abiria wote wanaofika mpakani hapo watalazimika kunawa mikono kwa maji tiririka na taratibu zingine kufuatwa ikiwemo kupimwa joto na kupatiwa vipeperushi vyenye ujumbe kuhusu masuala ya afya.

Amesema, “Abiria anapofika hapa kwanza kabisa ananawa mikono kwa maji tiririka na hatua zinazofuata ni vipimo kisha tunatoa vipeperushi pamoja na elimu ya afya kwa wasafiri wote wanaoingia katika mpaka huu.”

Kwa upande wake Afisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Kituo cha Rusumo, Mohammed Mnonda amesema kitengo cha afya kituo cha utoaji wa huduma kwa pamoja Rusumo, kimepewa jukumu la kuratibu shughuli zote zinazohusu afya, ikiwemo kupima abiria na kutoa elimu juu ya magonjwa mbalimbali ya mlipuko.

Mmoja wa abiria, katika mpaka huo kati ya Tanzania na Rwanda, Semakura Athuman amesema ana uelewa kuhusu ugonjwa wa Ebola kutokana na serikali kupitia Wizara ya Afya, Idara ya Kinga, Kitengo cha Elimu ya Afya kwa Umma kuweka mkazo wa utoaji wa elimu kila kona ya Tanzania.

Rais Samia ahitimisha mbio za Mwenge wa Uhuru
Wizara yatadhaharisha matumizi, wizi wa mtandao