Wawakilishi pekee wa England katika michuano ya UEFA Europa League, Arsenal wamepangwa kukutana na Atletico adrid ya Hispania katika mchezo wa nusu fainali.
Wawili hao wamekutanishwa baada ya kuchezeshwa droo ya nusu fainali leo mchana katika ukumbi wa mikutano wa shirikisho la soka barani Ulaya UEFA nchini Uswiz.
Arsenal wataanzia nyumbani Aprili 26 kwa mechi ya mkondo wa kwanza kabla ya kurudiana na Atletico May 3 2018.
Arsenal walifanikiwa kufuzu hatua ya nusu fainali usiku wa kuamkia leo, baada ya kuambulia matokeo ya sare ya bao moja kwa moja dhidi ya CSKA Moscow ya Urusi, na hivyo kupata ushindi wa jumla wa mabao sita kwa matatu.
Kwa upande wa Atletico Madrid walifuzu hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo, licha ya kufungwa bao moja kwa sifuri na Sporting CP ya Ureno usiku wa kuamkia leo.
Kabla ya mchezo huo Atletico Madrid walikua wana akiba ya ushindi wa mabao mawili kwa sifuri walioupata katika kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza uliochezwa juma lililopita.
Mchezo mwingine wa nusu fainali utakua kati ya Olympic Marseille ya Ufaransa watakaoanzia nyumbani dhidi ya Salzburg ya Ujerumani.
Olympic Marseille wamefuzu hatua hiyo kwa kuifunga RasenBallsport Leipzig mabao matano kwa mawili usiku wa kuamkia hii leo, lakini katika mchezo wa mkondo wa kwanza wafaransa hao walikubali kichapo cha bao moja kwa sifuri.
Salzburg ya Ujerumani usiku wa kuamkia leo ilifungwa na SS Lazio ya Italia mabao manne kwa mawili, lakini ushindi wa mabao manne kwa moja uliopatikana juma lililopita uliwasaidia kuvuka na kutinga nusu fainali.
Michezo ya nusu fainali ya UEFA Europa League imepangwa kuchezwa April 26 na Mei 03.