Serikali imeeleza hatua zilizochukuliwa kufuatia hasara iliyojitokeza kwa Serikali kupitia Kampuni ya mafuta ya TANOIL, ikiwemo ya kuwasimamisha kazi wafanyakazi wanne wa TANOIL.
Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga ameyasema hayo kwa niaba ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko wakati akitoa ufafanuzi wa hoja zilizowasilishwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na Mashirika ya Umma – CAG.
Amesema, Serikali inatambua umuhimu wa Sekta ya Mafuta nchini kwa uchumi wa nchi na ndio maana imechukua hatua kwa wote waliohusika kusababisha hasara ya takribani shilingi bilioni 7 kwa TANOIL, ametaja hatua nyingine iliyochukuliwa ni Kampuni zilizosababisha hasara hiyo kupisha TAKUKURU kufanya kazi yake.
“Nipende kuwataarifu waheshimiwa Wabunge kuwa Serikali kupitia Wizara ya Nishati imeshachukua na inaendelea na hatua za ndani kufuatia TANOIL kusababisha hasara kwa Serikali,” amesema Waziri Kapinga.
Bunge linaendelea na majadiliano ya ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na Mashirika ya Umma (CAG).