Saa chache zikisalia kabla ya mchezo wa mzunguuko wa pili wa Ligi Kuu dhidi ya Dodoma Jiji FC, Kiungo Mshambuliaji wa Mabingwa wa ligi hiyo Simba SC, Peter Banda ametoa ufafanuzi wa picha iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii ikimuonesha akiwa na Mshambuliaji na nahodha wa timu hizo John Raphael Bocco.

Picha ya wawili hao ilisambaa kwa kasi dakika chache baada ya kuwekwa kwenye kurasa za mitandao ya kijamii za Simba SC, ambapo ilitoa tafsiri tofauti kutoka kwa wadau wa soka nchini.

Banda amesema baada ya kufanya mazoezi ya mwisho jana Alkhamis (Septamba 30) kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma, Bocco alimfuata na kumwambia atulize akili acheze mpira, kwa sababu Wanasimba wana matumaini makubwa juu yake.

Banda amesema kitendo cha Bocco kumfuata na kuongea naye, kimemuongezea hamasa na hali ya kujiamini na anaamini kila kitu kitakaa sawa na ushindi utapatikana leo Ijumaa (Okotoba Mosi).

“Nahodha alikuja kuongea nami na kikubwa ameniambia niendelee kujituma na kutuliza akili kwa kuwa timu inahitaji ushindi na kwangu hilo ni jambo kubwa na linanifanya niongeze jitihada kila nitakapopata nafasi ya kucheza,” amesema.

Katika hatua nyingine Banda amesema timu yao inahitaji ushindi na wao kama wachezaji watajitahidi kuhakikisha hilo linafanikiwa na kuwapa mashabiki furaha.

“Tunahitaji kushinda kwenye mchezo wa kesho ni muhimu kwetu na wachezaji tunalijua tutapambana hadi mwisho kuhakikisha tunawapa mashabiki wetu furaha,” amesema Banda.

Simba ilianza kwa sare ya 0-0 dhidi ya Biashara United Mara iliyokua nyumbani Uwanja wa Karume mjini Musoma mkoani Mara siku ya Jumanne (Septemba 28), huku Bocco akikosa mkwaju wa Penati dakika za lala salama.

Makamu wa Rais wa Benki ya dunia kanda ya Afrika Mashariki amaliza ziara yake Nchini
Nahodha Geita Gold atamba kuibomoa Young Africans