Tetenasi ni ugonjwa unaosababishwa na bakteria wanaoitwa (Clostridium tetani), wadudu hawa wanapatikana katika mazingira yanayotuzunguka mfano, ardhi, misumari au vitu vyenye ncha, vinyesi vya baadhi ya wanyama nk.

Bakteria hawa wa tetenasi wanaweza kuishi katika mazingira kwa miaka mingi na pia wanapenda vidonda, ndio maana wanaingia mwilini kupitia vidonda au mikwaruzo, huku dalili za Tetenasi zikitokea siku 4 hadi 14 baada ya kupata jeraha.

Aina za Tetenasi.

Tetenasi imegawanyika sehemu mbili ambazo ni i. Tetenasi inayotokea kwa watu wazima (Adult), ii. Tetenasi ya watoto (Neonates).

Nani yupo hatarini kupata tetenasi?
Kwa watu wazima (Adults), ipo hivi, ikiwa umeumia na kupata jeraha au kidonda sehemu ya mwili wako uko katika hatari ya kupata ugonjwa huu hatari wa tetenasi na ikiwa umetobolewa na msumari basi tambua kwamba una zaidi ya asilimia 32 za kupata tetenasi.

Ikiwa umeungua, au watu wanaojidunga sindano za madawa ya kulevya, au watu wanaojiwekea tattoo, watu wenye magonjwa ya meno, wapo katika hatari ya kupata ugonjwa huu na hata Kisukari ni moja ya hali inayoweza kukusababishia tetenasi.

Aidha, upasuaji (Surgery), isiyo salama, mfano matumizi ya vyombo visivyo salama (unsterilized), kwa watoto na kama mama mjamzito hatapata chanjo ya tetenasi au kujifungulia nyumbani, yupo kwenye hatari ya kumsababishia mtoto mchanga kupata tetenasi.

Dalili za Tetenasi.
i. Kukakamaa kwa misuli, mdomo kushindwa kufunguka (lock-jaw)
ii. Kutokwa na jasho jingi, homa kali
iii. Kushindwa kumeza kwasababu ya kukakamaa kwa misuli.
iv. Kutokwa na udenda (drooling).
v. Kupata matatizo ya kupumua.

Kinga.
Tafadhali nenda Hospitalini au kituo cha afya mara baada ya kupata jeraha lolote ili kupata chanjo ya tetenasi na kwa wafanyakazi wa afya, ni muhimu kupata chanjo ya tetenasi kwasababu ya mazingira hatarishi ya kazi.

Kwa mama mjamzito, tafadhali hakikisha unapata chanjo zote za tetenasi ili kujikinga na pia kumkinga mtoto. Pia unapoona dalili za uchungu hakikisha unawahi ukajifungulie kituo cha afya mapema.
Epuka majeraha yasiyokua ya lazima, vaa viatu, weka vitu vyenye ncha kali mbali na watoto.

@Shukran kwa Dkt. habelnoah.

Diwani alala chini akimuomba Waziri utatuzi kero ya Maji
Sitasahau nilivyovuliwa Uwaziri - Kitwanga