Mlinda Lango chaguo la Kwanza katika kikosi cha Simba SC Aishi Salum Manula, anatarajia kujiunga na wachezaji wenzake katika mazozi ya pamoja, wakato wowote juma hili.

Taarifa njema za kurejea kwa Mlinda Lango huyo zimekuja, baada ya kikosi cha SImba SC kurejea jijini Dar es salaam jana Jumatatu (Septemba 18) kikitokea Ndola, Zambia, kilipocheza mchezo wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Power Dynamos na kupata sare ya mabao 2-2.

Aishi Manula aliumia nyonga Aprili 7, mwaka huu kwenye mchezo wa Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ dhidi ya Ihefu, jeraha lililosababisha kufanyiwa upausaji na kukaa nje ya uwanja kwa kipindi kirefu.

Mwanzoni mwa mwezi huu, Mlinda Lango huyo alianza mazoezi ya viungo, gym na yale ya kisayansi na kuimarika kidogo kidogo na juma hili atafanyiwa vipimo vya mwisho kujua maendeleo yake kisha baada ya hapo ataruhusiwa kujiunga na timu kwa ajili ya mazoezi ya jumla na utakuwa uamuzi wa Kocha Robertinho kama amtumie au hapana.

Wakati Manula akiwa majerahi, Simba SC ilihaha kutafuta mrithi wake ndipo ikamsajili Mbrazil, Jeferson Luiz ambaye alipata majeraha wakati timu ikiwa kwenye maandalizi ya msimu huu Uturuki na kuachana naye kisha ikamsajili Ayoub Lakred kutoka Morocco sambamba na Hussein Abel kutoka KMC, walioingia kikosini kuongeza nguvu kwa Ally Salim na Feruz Teru lakini wote wanaonekana kutokuwa na viwango sahihi.

Hata hivyo, Salim ndiye aliyepata nafasi kubwa ya kucheza lakini bado hakufikia ubora wa Manula na hata Ayoub alipopewa nafasi kwenye mchezo dhidi ya Dynamos alifanya makosa ambayo yaliwafanya mashabiki wa Simba SC kumkumbuka Manula.

Daktari wa Simba Edwin Kagabo amesema hali ya Manula inaendelea vizuri na amekuwa akifanya kwa usahihi programu anazopewa na muda wowote anaweza kujiunga na wenzake.

“Alipewa mazoezi tiba na kuyafanya vizuri, ameimarika kwa haraka sana na baada ya vipimo vya mwisho baada ya timu kurejea Dar es salaam anaweza kujiunga na wenzake,” amesema Kagabo.

Kwa maana hiyo kama Manula ataanza mazoezi juma hili, basi kuna uwezekano mkubwa wa kuwepo kikosini kwenye mechi ya kwanza ya African Football League dhidi ya Al Ahly kutoka Misri mchezo utakaopigwa Oktoba 20, mwaka huu Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Wasaidizi wa kazi Nyumbani waivuta shati Serikali
Kocha Gamondi afichua siri ya ukuta wake