Serikali ya Ufaransa imeahidi kutoa Euro milioni 150, kwa ajili ya kuendeleza mradi wa awamu ya tano wa ujenzi wa mradi wa mabasi ya mwendokasi jijini Dar es Salaam.

Ahadi hiyo imetolewa na Balozi wa Ufaransa hapa nchini, Mhe. Frederic Clavier wakati alipokutana kwa mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi, katika ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.

Prof. Kabudi amesema kuwa mazungumzo yake na Balozi Clavier yalijikita katika utekelezaji wa mambo waliyokubaliana wakati alipofanya ziara ya kikazi mwezi Februari nchini Ufaransa.

“Leo katika mazungumzo yangu mimi na Balozi tumejadili mambo mbalimbali likiwemo suala la Shirika la Maendeleo la Ufaransa kutoa fedha kwa ajali ya kuendeleza mradi wa awamu ya tano wa ujenzi wa mradi wa mabasi ya mwendokasi jijini Dar es Salaam,” amesema Prof. Kabudi.

Pamoja na mambo mengine, Prof. Kabudi amesema kuwa wamejadili kuhusu miradi ya maendeleo katika sekta ya nishati, maji, afya na kilimo.

“Pia tumejadili kuhusu ushiriki wa Ufaransa katika kuisaidia Tanzania katika uchumi wa buluu, ambapo Shirika la Maendeleo la Ufaransa limeahidi kusaidia Tanzania bara na Zanzibar katika kuendeleza uchumi wa buluu na hasa kuongeza uwezo wa Tanzania kuvua na kuchakata samaki,” ameongeza Prof. Kabudi.

Kwa upande wake Balozi wa Ufaransa Nchini, Frederic Clavier amesema kuwa kikao chake na Waziri Kabudi ni mwanzo wa hatua mpya ya ushirikiano kati ya Tanzania na Ufaransa.

“Nchi ya Tanzania ni nchi ya demokrasia na amani,ambapo inatoa fursa ya kuwekeza katika miradi ya maendeleo, Ufaransa itaendelea kuwa pamoja na Tanzania katika kuhakikisha kuwa inasonga mbele kimaendeleo,” amesema Balozi Clavier. 

Kiswahili chapendekezwa kutumika rasmi SADC
Habari kubwa kwenye magazeti leo, Machi 9, 2021