Aliyewahi kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya Ufaransa Henri Michel, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 70.
Michele alibahatika kukiongoza kikosi cha Ufaransa katika michuano ya Olimpiki mwaka 1984 na kufanikiwa kutwaa medali ya dhahabu, mjini Los Angeles nchini Marekani.
Mwaka huo huo Michele alibahatika kukifikisha kikosi cha Ufaransa katika hatua ya nusu fainali ya kombe la dunia nchini Mexico, na kwa bahati mbaya alipoteza dhidi ya Ujerumani Magharibi kwa kufungwa mabao mawili kwa sifuri, kabla ya kuichapa Ubelgiji mabao manne kwa mawili kwenye mchezo wa kuwania mshindi wa tatu.
Shirikisho la soka nchini Ufaransa FFF, limethibitisha kifo cha gwiji huyo ambaye alifanikiwa kucheza michezo 500 akiwa na klabu ya Nantes na kutwaa ubingwa wa Ligue 1 mara tatu.
Kwa upande wa timu ya taifa Michele, atakumbukwa kwa mchango wake alioutoa katika michezo 58 aliocheza kuanzia mwaka 1967 hadi 80 na kufunga mabao manne.
Mbali na kuifundisha timu ya taifa ya nchi yake, Michele pia aliwahi kuinoa timu ya taifa ya Cameroon (1994), Morocco (1998) na Ivory Coast (2006).
Kazi yake ya mwisho aliyoifanya katika tasnia ya ukufunzi ilikua nchini Kenya akikinoa kikosi cha timu ya taifa ya nchi hiyo (Harambee Stars) mwaka 2012.