Ufunguo wa selo ya gereza ya Kisiwa cha Robben alikofungwa Nelson Mandela unatarajiwa kurudishwa Afrika Kusini badala ya kupigwa mnada nchini Marekani.
Mnada huo ulikuwa ufanyike New York tarehe 28 Januari hadi Waziri wa Utamaduni wa Afrika Kusini Nathi Mthethwa alipopinga.
“Ufunguo huu ni wa watu wa Afrika Kusini,” alisema.
Bw Mthethwa alisema jumba la mnada la Guernsey lilikubali kurudisha ufunguo huo nchini Afrika Kusini na pia kusitisha uuzaji wa vitu vingine vilivyokuwa vya Mandela.
Mnada huo ulikuwa wa kuchangisha fedha kwa ajili ya bustani ya kumbukumbu na makumbusho karibu na eneo la maziko ya Mandela.
Hizi ni pamoja na mchoro asilia wa Mandela The Lighthouse, Robben Island, pamoja na baiskeli ya mazoezi aliyoruhusiwa kutumia na raketi ya tenisi gerezani
“Ufunguo unaashiria historia chungu ya Afrika Kusini huku pia ikiwakilisha ushindi wa roho ya mwanadamu dhidi ya uovu,” Mthethwa alisema katika taarifa.
Ufunguo huo ulikuwa umeuzwa na Christo Brand, mlinzi wa zamani wa jela ya Mandela katika jela hiyo yenye sifa mbaya. Wawili hao walikuwa marafiki wa karibu.
Mandela alikaa jela miaka 27 kwa kufanya kampeni ya kukomesha utawala wa wazungu wachache, Miaka kumi na minane kati ya hiyo ilikuwa kwenye Kisiwa cha Robben, kisiwa kilicho karibu na Cape Town.
Mandela aliachiliwa kutoka gerezani mwaka wa 1990 wakati Afrika Kusini ilipoanza kuachana na ubaguzi mkali wa rangi (apartheid).
Mnamo 1994, alikua rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini baada ya uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia nchini humo, na bado anabaki kuwa mwanasiasa wa kitaifa.
Alihudumu kwa muhula mmoja kama rais, akiondoka madarakani mnamo 1999, hata hivyo aliaga dunia mwaka 2013 akiwa na miaka 95.