Visa vya wagonjwa wa homa kali ya mapafu, Covid 19 nchini Uganda vimefikia 114 baada ya madereva wengine kukutwa na maambukizi ya virusi vya Corona vinavyosababisha ugonjwa huo.
Wizara ya afya imetangaza visa vipya 13, idadi ambayo ni kubwa zaidi kurekodiwa kwa siku moja ambapo wagonjwa wote ni madereva wa malori ambapo 7 ni Wakenya, 4 ni Waganda na wawili ni Watanzania.
Wagonjwa hao walithibitika baada ya sampuli 2,421 za madereva kufanyiwa vipimo. Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dkt. Diana Atwine amesema wanafanya kazi kwa bidii kuhakikisha upimaji unaanza mipakani.
Aidha, Rais Yoweri Museveni amesema amewakaribisha Viongozi wa Dini Ikulu leo kwa ajili ya maombi ya kitaifa, amewataka wananchi kuiombea Uganda huku wakizingatia tahadhari za kujikinga na maambukizi.