Sheikh Mohammed Mutumba aliyemuoa mwanamume mwenzake akidhani ni mwanamke amefutwa kazi na baraza kuu la Waislamu nchini Uganda.

Baraza hilo linasisitiza kuwa kuna dosari kubwa kwa upande wa imam huyo na hastahili kuendelea na kazi yake huku mjadala kuhusu kama kweli alifahamu jinsia ya bi harusi wake wiki mbili zilizopita alipofanya nikka naye ukiwa bado unaendelea.

Sheikh Mutumba anadai kuwa alipata mshtuko wiki mbili baada ya kugundua kuwa mke aliyemuoa aliyekuwa akivalia vazi la hijab kila wakati na anafahamika kama Swabullah Nabukeera alikuwa ni mwanaume anayeitwa Richard Tumushabe.

Ukweli kuhusu jinsia yake ulibainika baada ya polisi kumkamata Tumushabe kwa madai ya wizi wa televisheni na nguo za jirani yake.

Imeelezwa kuwa wakati polisi wakifanya shughuli zao za kila siku, askari wa kike alimkagua sehemu zake za mwili kabla hajampeleka jela, na kuwashangaza maafisa wa polisi kuwa mtuhumiwa huyo aliweka nguo katika sidiria ili aonekane ana matiti.

Sheikh Mutumba ambaye ni imam wa msikiti uliopo kijiji cha Kyampisi, kaskazini magharibi mwa mji mkuu wa Uganda, Kampala alidai kuwa hajafanya naye tendo la ndoa mke wake huyo tangu amuoe kwa sababu alisema kuwa alikuwa ana matatizo ya kiafya yaliyomfanya kuendelea kupata hedhi na ilimbidi amvumilie mpenzi wake.

Msemaji wa polisi mkoa maalumu wa polisi wa Ssezibwa, Hellen Butoto amefahamisha BBC kwa njia ya simu kuwa mtuhumiwa bado amehifadhiwa kituo cha polisi Kayunga na amefunguliwa mashitaka.

Kigwangalla ahoji bilioni 4 alizotumia Mo kwa wanasimba
Video: Sakata la Meya Dar Sarakasi tupu, Joto sasa lazidi kuzua kihoro