Rais wa Uganda, Yoweri Museveni ametangaza visa vipya 11 vya ugonjwa wa corona (Covid-19) nchini humo, wote wakiwa wanakwaya wa kwaya maarufu inayojulikana kama ‘Watoto Children’s Choir’ ambapo mpaka sasa Uganda imethibitisha kuwa na wagonjwa 44.
Kupitia matangazo ya televisheni, Rais Museveni amesema kuwa wagonjwa wote wapya walikuwa karantini baada ya kurejea kutoka ughaibuni , ingawa hakueleza afya zao zikoje kwa sasa na walikuwa wametoka taifa gani.
Aidha, kwaya hiyo mara nyingi huwa inatumbuiza katika nchi za ughaibuni kama Marekani, Canada na Uingereza.
Katika hotuba yake kwa Taifa hilo, Jumatatu, Machi 31, 2020, Rais Museveni alipiga marufuku usafiri wa kutumia magari binafsi na bodaboda kuanzia saa nne usiku. Rais huyo ametangaza masharti zaidi ya kukabiliana na kuenea kwa virusi vya corona.
Mtu yeyote anayehitaji huduma za dharura za kiafya kama vile kujifungua au kufanyiwa upasuaji anatakiwa kupata idhini kutoka kwa maafisa wa serikali katika ngazi ya Wilaya kabla ya kutoka nyumbani, kwa mujibu wa masharti hayo.
Rais amesema kuwa wakati serikali awali ikiweka marufuku ya watu kukusanyika, bado kumekuwa na mianya ya kusambaa kwa virusi.
Ingawa alieleza kuwa kati ya watu 33 waliothibitishwa kuwa na maambukizi, watatu pekee walikuwa wasafiri waliopata maambukizi wakiwa safarini nje ya Uganda.