Serikali ya Uganda, imesema mwishoni mwa mwezi huu (Novemba), itapeleka wanajeshi 1,000 katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kujiunga na kikosii cha kikanda kusaidia kurejesha utulivu kama ilivyofanya nchi ya Kenya.
Kwa mujibu wa Msemaji wa jeshi la Uganda, Felix Kulayigye amesema kikosi hicho kitakuwa cha tatu kuwasili nchini Congo, baada ya Kenya na Burundi kutuma wanajeshi wake kwenye eneo hilo la mashariki ili kutoa msaada wa mapambano.
Kuhusika kwa Uganda katika kikosi cha kikanda, kunapingwa na baadhi ya maafisa wa Congo na makundi ya kiraia yanayoituhumu nchi hiyo kuhusika katika vita vinavyoikumba DRC kama wanavyoituhumu nchi ya Burundi.
Hata hivyo, kupelekwa kwa kikosi hicho, ni sehemu ya makubaliano na Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC, ili kulisaidia jeshi la DRC kuzima uasi wa kundi la M23 unaofanyika katika eneo hilo la mashariki mwa DRC.