Gazeti la Daily Monitor limeripoti kuwa Wakaguzi kutoka Umoja wa Ulaya (EU) wameidhinisha Uganda kutuma bidhaa za bangi barani Ulaya,

Bangi itakayotumwa kwenye soko la Ulaya hata hivyo si kwa matumizi ya starehe kama uvutaji bali ni kwa ajili ya matibabu.

Kwa mujibu wa Gazeti la Daily Monitor, Mainspekta wa bidhaa za matibabu zitokanazo na bangi kutoka Uholanzi walikagua mashamba ya bangi kwenye wilaya za Hima na Kasese kati ya Julai 29 na Agosti 4.

Maafisa hao kabla ya kuondoka Uganda walikabidhi cheti cha kukidhi vigezo kampuni ya Industrial Globus Uganda Ltd kwa kipindi cha Agosti 6, 2019 mpaka Agosti 5, 2020.

Kwa upande wake mkurugenzi wa kampuni hiyo, Benjamin Cadet amelithibitishia gazeti hilo kuwa EU wamewapa idhini ya kusafirisha bangi Ulaya.

“Baada ya EU kuthibitisha bidhaa zetu, usafirishwaji na mnyororo wote wa uzalishaji kuanzia kupanda mpaka kuvuna kwa bangi, utafanyika kikamilifu nchini Uganda na kupelekwa kwenye masoko ya Ulaya,”amesema Cadet

Takribani kampuni 50 zimeomba kibali Wizara ya Afya kuungana na kampuni ya Industrial Globus Uganda Ltd ili kuzalisha bangi kwa ajili ya matibabu.

Bangi inayozalishwa Uganda katika shamba la wilayani Kasese ina virutubisho vya Cannabinol (CBD) na Tetrahydrocannabinol (THC) ujazo wa 2.7mg THC na 2.5mg CBD ambapo virutubisho hivyo vimepasishwa Ulaya, Marekani na Canada.

Uganda ilishindwa kusafirisha bangi ya thamani ya dola 600 milioni kwenda Canada na Ujerumani mwezi Julai mwaka huu baada ya kampuni ya Industrial Globus Uganda Ltd kutokuwa na cheti kutoka EU.

Uganda ndio nchi pekee Afrika Mashariki ambayo imehalalisha uzalishaji wa bangi, japo kwa matumizi ya kiafya.

Rais wa kwanza wa Gambia afariki dunia
Aihama nchi yake kutoroka ubaguzi wa rangi