Watafiti katika Chuo Kikuu cha Makerere wakishirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Virusi nchini Uganda (UVRI), wamegundua aina mbili za jeni zinazoongeza hatari ya kupata ugonjwa wa figo.
Kiongozi wa utafiti huo Mwanasayansi Christopher Kintu amesema walichambua data za washiriki 80,027 toka vikundi vitatu vya watu ulimwenguni, na kugundua lahaja za jeni kwenye SLC22A2 na GATM, ambazo ni za kipekee.
“SLC22A2 ni jeni ya kuweka misimbo ya protini ambayo inawajibika kuondoa sumu na kimetaboliki ya dawa kwenye figo, ambapo namba za jeni za GATM za kimeng’enya zinahusika katika kimetaboliki,” alisema Kintu.
Watafiti hao wanasema matokeo yanalenga uchukuaji wa hatua za kuzuia ugonjwa huo na kuwashauri wenye vinasaba kuendana na mabadiliko ya mtindo wa maisha, utakaopunguza hatari ya kupata ugonjwa huo.
“Tunaweza kutumia chembe za watu kutabiri ugonjwa kabla hata haujatokea na ili kufanya hivyo tunapaswa kupata alama za hatari za polygenic na tunawashauri kupunguza hatari ya kupata ugonjwa huo kwa kuepuka pombe au kufanya mazoezi,” aliongeza.
Kwa upande wake mmoja wa washiriki wa utafiti huo Prof. Segun Fatumo amesema kuna haja ya kuwajumuisha waafrika katika tafiti za genomic ili kupata matokeo bora yatakayosaidia kuepukana na maradhi hayo.
“Hivi sasa, tafiti za genomic zinajumuisha watu wenye asili ya Uropa na hii ina maana alama za hatari za kijeni katika kutabiri ugonjwa zinatumika kwa wakazi wa Ulaya wakati sisi tupo Afrika hii si sahihi,” alisema Fatumo.
Kuenea kwa ugonjwa wa figo nchini Uganda, kumesababisha karibu asilimia 6.8 ya raia wa nchi hiyo kusafiri mataifa ya nje kwenda kupandikiza figo kwa gharama kubwa kutokana na ukosefu wa vifaa nchini Uganda.