Shirika la Afya ulimwenguni (WHO), limethibitsha ripoti ya nchi 12 zilizoonesha matukio 80 ya
uwepo wa ugonjwa wa Monkeypox na kwamba bado wanachunguza madai mengine 50 ya
maradhi hayo na kuonya Mataifa Ulimwenguni kuchukua tahadhari.

Kwa mujibu wa Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa WHO kanda ya Ulaya Dkt. Hans Henri Kluge
imetaja nchi hizo kuwa ni Ujerumani, Sweden, Ubelgiji, Ufaransa, Italia, Ureno, Uhispania na
Uingereza.

“Maambukizi ya ugonjwa huo unaoharibu ngozi pia yamethibitishwa katika nchi za Ulaya,
Amerika, Canada na Australia lakini kwa Afrika unapatikana katika sehemu za mbali za Afrika ya
Kati na Magharibi,” ameongeza Kluge.

Ugonjwa huo ambao unasababisha na virusi kutoka kwa Wanyama kwenda kwa binadamu barani Afrika unatajwa kutokea katika jamii zilizopo karibu na misitu ya Afrika ya kati na Magharibi kuliko na hifadhi za Wanyama.

Dkt. Kluge amesema matukio ya wagonjwa wa Monkeypox yamegunduliwa katika kliniki
maalumu za magonjwa ya zinaa na kwamba maambukizi hayahusishi muingiliano wa safari
ingawa mapenzi ya jinsia moja kwa wanaume ni moja ya sababu.

“Hata hivyo dalili za wagonjwa waliogundulika barani ulaya zinaonesha kufanana na zile
zilizoripotiwa siku za karibuni katika nchi za Australia, Canada na Marekani ila hakuna uhusiano wa kimaambukizi kulingana na muingiliano wa wasafiri,” amefafanua Kluge.

Mtoto mwenye Monkeypox

Aidha Dkt. Kluge amebainisha kuwa WHO inaendelea kufanya uchunguzi kwa nchi ambazo
ugonjwa huo umeibuka ili kupata taarifa zitakazosaidia ugunduzi wa matukio mengine ingawa mpaka sasa haijulikani kiwango cha maambukizi kilichopo kwenye jamii.

“Kwa sasa dalili ni ndogo na wengi wa walio ambukizwa watapona ndani ya wiki chache bila
matibabu ila ugonjwa huu unaweza kuwa mkali zaidi hasa kwa watoto wadogo, wanawake
wajawazito na watu ambao hawana kinga mwilini.” ameelekeza DKt. Kluge.

Ugonjwa wa Monkeypox huambukizwa kwa kugusana na mtu mwenye vidonda kwenye ngozi,
kuvuta hewa yenye matone ya mtu aliye na ugonjwa huo au maji maji ya mwilini, kujamiiana, au kuchangia vitu na mtu aliyeambukizwa.

WHO inaelekeza kuwa dalili za ugonjwa huo zinaweza kuwa ndogo lakini vipele vinavyotokea
kwenye ngozi huwasha na kuleta maumivu na imetoa wito kwa yeyote aliye na dalili za vipele
visivyo vya kawaida kuwahi hospitali ili kupata ushauri wa watoa huduma za afya.

Bado hakuna tiba maaalum ya Monkeypox lakini chanjo ya ugonjwa wa ndui inatajwa kutoa kinga kwa asilimia 85 kwa kuwa virusi hivi viwili ni familia moja na uwezekano wa kuambukizwa ni mdogo.

Rais Samia amuapisha Mwalimu wake
Wakwamishaji miradi Kigoma kukiona