Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha limefanikiwa kukamata Bastola moja aina ya CZ 75 LUGER yenye namba za usajili A487385 pamoja na risasi 71 za bastola iliyokuwa inatumiwa na wahalifu ambao walikimbia eneo la tukio.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Kamanda wa Polis Mkoani humo, imeeleza kuwa silaha hiyo pamoja na risasi, ilipatikana katika nyumba iliyopo maeneo ya Ilkyurei, Kata ya Kiranyi, wilaya ya Arumeru, baada uwepo wa taarifa toka kwa wananchi kuhusiana na wahalifu hao.
Katika tukio la pili, Polisi pia imewakamata watuhumiwa 11 wa dawa za kulevya wakiwa na mirungi bunda 528 zenye uzito wa kilogramu 162.97 ambayo waliyokuwa wakiisafirisha kwa kutumia vyombo vya moto ikiwemo gari pamoja na pikipiki na kwamba upelelezi juu ya matukio hayo unaendelea ili kuwafikisha watuhumiwa Mahakamani.
Aidha, katika tukio la tatu, Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, limefanikiwa kumfikisha mahakamani mtu mmoja Raphael Mollel (27), mkazi wa kijiji cha Lashaine wilaya ya Monduli kwa tuhuma za kumbaka mwanafunzi (08), wa darasa la pili ambaye alikutwa na hatia na Machi 6, 2023 alihukumiwa kifungo cha maisha jela.